1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini kupambana na LRA

Kabogo Grace Patricia27 Septemba 2010

Mipango ya mapambano hayo itahusisha kuyapatia silaha makundi ya wapiganaji wa kijamii.

https://p.dw.com/p/PNqa
Kiongozi wa Lord's Resistance Army-LRA, Joseph Kony.Picha: picture-alliance/ dpa

Sudan Kusini ina mpango wa kuyapa silaha makundi ya wapiganaji ya kijamii ili yaweze kupambana na kundi la waasi la Uganda la Lord's Resistance Army-LRA. Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa Gavana wa jimbo ambalo linakabiliwa zaidi na mashambulio ya waasi wa LRA.

Gavana wa jimbo hilo linalokabiliwa zaidi na mashambulio ya LRA, la Equata Magharibi, Joseph Bakasoro amesema makundi ya kujilinda yanayojulikana kama ''Arrow Boys'' ambayo yana silaha za jadi kama vile mapanga, tayari wanalinda jamii zinazoshambuliwa na wapiganaji wa LRA, kutokana na vikosi vya usalama vya Sudan kutoingia sana katika maeneo ya misituni ambako waasi hao wamekimbilia. Bwana Bakasoro amesema bunge la Sudan Kusini limetenga kiasi cha dola milioni mbili kwa ajili ya kununua bunduki, vifaa vya mawasiliano na kugharamia mafunzo ya kijeshi ya wapiganaji wa makundi hayo ya kijamii.

Kundi la LRA linawalenga kwa makusudi raia pamoja na vijiji kwa mashambulio ya kila wiki na watu huwa wanaathiriwa vibaya. Maelfu ya watu wameuawa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita ya mapigano tangu kiongozi wa kundi hilo la Lord's Resistance Army-LRA, Joseph Kony alipoanzisha mapigano, awali dhidi ya serikali ya Uganda. Tangu waasi hao walipofukuzwa Uganda, wamekimbilia katika maeneo ya misitu mikubwa na kulidhibiti eneo la Sudan Kusini, kaskazini-mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mafunzo kwa makundi hayo

Bwana Bakasoro, amebainisha kuwa makundi hayo ya wapiganaji wa kijamii yatapatiwa mafunzo na kuwa karibu na jeshi la Sudan Kusini linaloundwa na wapiganaji wa zamani wa kundi la waasi la Sudan Peoples' Liberation Army-SPLA. Ameongeza kusema kuwa pindi kundi la LRA litakaposhindwa na suala la waasi kumalizika kabisa, SPLA wataenda katika maeneo yao na kukusanya silaha. Wengi wana hofu kuwa LRA wanaweza kusababisha kutokuwepo kwa hali ya utulivu wakati wa kura ya maoni mwezi Januari mwakani, wakati eneo la Sudan Kusini litakapopiga kura kuamua iwapo lijitenga na serikali ya Khartoum au liendelee kuwa sehemu ya serikali hiyo.

Vitendo vya kikatili vinavyofanywa na waasi wa LRA ni pamoja na mauaji, ubakaji na kuwalazimisha watoto kujiunga na kundi hilo. Umoja wa Mataifa umesema kuwa kuanzia mwezi Januari, kundi hilo limewalazimisha zaidi ya watu 250,000 kuyakimbia makaazi yao Sudan Kusini peke yake. Kundi hilo la waasi wa LRA, ambalo kiongozi wake anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC kwa makosa ya uhalifu wa kivita, limewaua, kuwateka nyara au kuwaacha bila makaazi maelfu ya wananchi wa nchi jirani za Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mwanzoni mwa mwezi huu, mkutano wa viongozi wa kidini na kisiasa kutoka katika nchi hizo tatu ambako waasi hao wanaendesha shughuli zao, walitaka kuwepo kwa maafikiano kuhusu mzozo huo baada ya jeshi kushindwa kuingilia katia mapigano hayo kwa miongo kadhaa. Jeshi la Uganda liliongoza operesheni ya kuwasaka viongozi wa LRA kuzunguka Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati, tangu lilipoanzisha mashambulio kutokana na kuvunjika kwa mazungumzo ya amani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri:Abdul-Rahman