1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yaombwa kutopoteza muda katika suala la amani

14 Mei 2018

Mjumbe wa Kimataifa Festus Mogae amesema Sudan Kusini haipaswi kupoteza nafasi katika mkutano unaokuja wa kutafuta amani hata kama makubaliano yaliyopita yalikiukwa mara kadhaa na pande zinazohasimiana.

https://p.dw.com/p/2xhoM
Festus Mogae
Picha: picture-alliance/ dpa

Licha ya makubaliano kadhaa ya kusimamisha mapigano, bado mapigano yameendelea nchini humo bila ya kusitishwa tangu vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka mwishoni mwa mwaka 2013 miaka miwili tu baada ya taifa hilo changa kabisa duniani kujipatia uhuru wake.

Majeshi yaliyotiifu kwa rais Salva Kiir yalipambana na majeshi yaliyotiifu kwa makamu wa rais wa zamani Riek Machar. Maelfu ya watu wameuwawa tangu mgogoro huo kuanza huku taifa hilo likikabiliwa na upungu mkubwa wa chakula. Hata hivyo serikali na makundi ya waasi walitia saini mpango wa kusitisha mapigano mwezi Desemba mjini Addis Ababa Ethiopia wakinuia kufufua makubaliano yaliyotiwa saini mwaka 2015. Lakini makubaliano hayo yalikiukwa saa kadhaa baada ya kutiwa saini.

Südsudan Riek Machar  Salva Kiir
Makamu wa zamani wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar na rais wa Sudan kusini Salva KiirPicha: picture-alliance/AP/J. Patinkin

Kwa sasa pande husika zitakutana tena mjini Addis Ababa kuanzia tarehe 17 hadi 21 mwezi Mei kujaribu kuanzisha tena mchakato wa kutafuta amani uliyoandaliwa na jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo ya nchi za kanda ya Afrika Mashariki na pembe ya Afrika IGAD.

"Nchi hii imekosa nafasi nyingi sana ya kuhakikisha kunakuwepo na amani ya kudumu na hatupaswi kukubali mkutano mwengine kukosa nafasi hiyo," alisema Festus Mogae, rais wa zamani wa Botswana katika hotuba yake. Mogae kwa sasa anaongoza kamisheni ya pamoja iliyoundwa kusimamia mchakato uliyofeli wa kutafuta amani nchini Sudan Kusini. Nchi hiyo pia imeunda mchakato wa mazungumzo ya kitaifa  wakati mapigano bado yanaendelea nchini humo.

Mogae amezishtumu pande hasimu kwa kukiuka haki za binadamu huku akiihimiza IGAD kuwachukulia hatua wale wote wanaoyumbisha au kuharibu makubaliano hayo. Ameongeza kuwa pande hizo hasimu zinaendelea kufanya uasi na kutekeleza ukiukwaji wa haki za binaadamu wakiwa na msamaha na kuitaka IGAD kuwachukulia hatua wahusika wanaotekeleza makosa hayo.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga