1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan mbili kurudi mezani wiki ijayo

Admin.WagnerD23 Mei 2012

Msuluhishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Sudan na Sudan Kusini, rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki, amesema mazungumzo ya amani baina ya nchini hizi yataanza tena wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/150R5
Marais Omar el Bashir na Salva Kiir
Marais Omar el Bashir na Salva KiirPicha: picture-alliance/dpa

Mbeki amesema kamati yake imepata baraka za marais wote, Omar el Bashir wa Sudan na Salva Kiir wa Sudan Kusini kwamba paneli za majadiliano zikutane wiki ijayo ingawa hakubainisha wazi ni siku gani majadiliano hayo yataanza.

Tangazo hilo la Mbeki limekuja muda mfupi baada ya Sudani Kusini kudai kuwa ndege za Sudan zilishambulia tena eneo moja la mpakani siku za Jumatatu na Jumanne. Mbeki alisema wajumbe kutoka pande zote watafanya marejeo ya maamuzi yaliyofanywa na Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Msuluhishi wa mgogoro huo Thabo Mbeki.
Msuluhishi wa mgogoro huo Thabo Mbeki.Picha: picture-alliance/dpa

Shinikizo kutoka jumuiya ya kimataifa
Azimio la Umoja wa Afrika lilitengeneza msingi wa matakwa ya Umoja wa Mataifa kwa Sudan na Sudan Kusini yaliyotolewa Mei 2 na kuzitishia nchi hizi vikwazo kama zisingetekeleza matakwa hayo. Lakini Nchi hizi zilishindwa kutekeleza sharti la kuanza mazungumzo kabla ya Jumatano iliyopita lililowekwa na Baraza la Usalama.Sudan Kusini ilisema ilikuwa tayari kuanza mazungumzo na kuituhumu Sudan kwa kuyakwamisha.

Thabo Mbeki, ambaye ni rais wa zamani wa Afrika Kusini, amekuwa akizunguka kati ya Sudan na Sudan Kusini tangu wiki iliyopita katika jitihada za kuyashinikiza mataifa hayo mawili kuerejea mazungumzo. Baada ya kukutana na rais Kiir siku ya Jumatatu, Mbeki alisema ni muhimu kwa kamati yake kuzikutanisha pande mbili haraka iwezekanavyo ingawa hakubainisha hasa ni siku gani majadiliano hayo yataanza.

Sudan ilijiondoa katika mazungumzo yaliokuwa yanaratibiwa na Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa baada ya Sudan Kusini kuteka eneo la Heglig atrehe 10 Aprili, ambalo linategemewa na Sudan kwa uchimbaji wa mafuta, baada ya mataifa hayo mawili kutengana Julai mwaka jana. Uvamizi huu wa Sudan Kusini ulisababisha mashambulizi makali ya angani kutoka kwa Sudan na kutishia kutokea kwa vita baina mataifa haya mawili.

Mtambo wa kusafishia mafuta ulioko eneo la Heglig.
Mtambo wa kusafishia mafuta ulioko eneo la Heglig.Picha: Reuters

Muktadha wa majadiliano
Mazungumzo ya wiki ijayo yatalenga kutafuta ufumbuzi wa masuala yaliobaki bila kupatia majibu baada ya uhuru wa Sudan Kusini ambayo ni pamoja na malipo yanayotokana na mafuta, hadhi ya raia wa nchi zote waliobakia katika kila upande baada ya uhuru, hadhi ya eneo la Abyei na pia kutafuta suluhu ya maeneo ya mpakani yanagombaniwa na mataifa haya mawili.

Waziri wa Mawasiliano wa Sudan Kusini, Barnaba Marial Benjamini, aliwambia waandishi wa habari siku ya Jumanne kuwa Sudan imeanza upya kuwashambulia na kudai kuwa mashambulizi hayo yanalenga eneo la Werguet lililoko kaskazini mwa jimbo la Bahr el Ghazal linalopakana na Darfur na kusema kuwa kama mashambulizi haya yataendelea, basi Sudan Kusini haitakuwa na budi kujibu.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.