Watuhumiwa wa uhalifu wa kivita kukabidhiwa ICC
11 Februari 2020Hayo yameelezwa na waziri wa habari Faisal Saleh aliyezungumza na shirika la habari la Reuters leo. Hata hivyo waziri huyo hakumtaja moja kwa moja aliyekuwa rais wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar al-Bashir, ambaye pia anatakiwa na mahakama hiyo.
Bashir aliondolewa kwa nguvu madarakani baada ya maandamano makubwa ya kumpinga mwaka jana. Lakini Afisa mwingine mwandamizi amesema kuwa serikali ya mpito ya Sudan imekubaliana na makundi ya waasi kumfikisha Bashir katika mahakama ya ICC.
Bashir ambaye alindolewa madarakani na jeshi mwaka jana kutokana na maandamano ya umma, anasakwa na ICC kwa mashitaka ya uhalifu dhidi ya binaadamu na mauaji ya halaiki yanayohusiana na mgogoro wa Darfur.
Tangu kuangushwa kwake Aprili, amekuwa kizuizini mjini Khartoum, kwa mashitaka ya ufisadi na mauaji ya waandamanaji.