1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Maandamano zaidi ya kupinga mapinduzi ya kijeshi

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
24 Januari 2022

Maelfu ya waandamanaji nchini Sudan wamejitokeza barabarani kudai urejeshwe madarakani utawala wa kiraia. Waandamanaji hao pia wanadai haki kwa watu waliouawa tangu mapinduzi ya kijeshi karibu miezi mitatu iliyopita.

https://p.dw.com/p/4618F
Sudan Khartum | Protest gegen die Machtübernahme durch das Militär
Picha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Umati huo wa watu ulikusanyika katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na waandamanaji walisikika wakipaza sauti kwa maneno ya kulikashifu jeshi wakati walipokuwa wanaelekea kwenye ikulu, eneo ambalo vikosi vya usalama vililifunga kabla ya maandamano hayo kuanza. Maandamano pia yamefanyika katika mji wa Wad Madani, ulio kusini mwa mji mkuu, Khartoum, na pia katika jimbo la mashariki la Gedaref. Sudan imekuwa inakumbwa na maandamano ya mara kwa mara tangu jeshi chini ya uongozi wa jenerali Abdel Fattah al-Burhan liliponyakua madaraka mnamo Oktoba, 25  mwaka uliopita.

Waandmanaji katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum wanaopinga mapinduzi ya kijeshi
Waandmanaji katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum wanaopinga mapinduzi ya kijeshiPicha: AFP/Getty Images

Mapinduzi hayo yalisambaratisha makubaliano ya kugawana madaraka kati ya viongozi wa kiraia na wa kijeshi. Makubaliano hayo ya kuunda serikali ya mpito yalifikiwa kwa tabu baada ya kuondolewa madarakani dikteta Omar al-Bashir mwaka wa 2019.

Takriban watu 73 wameuawa tangu yalipoanza maandamano hayo ya kupinga mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan. Mamia kadhaa ya watu wamejeruhiwa kulingana na madaktari wanaounga mkono vuguvugu la raia wanaotaka demokrasia.

Wiki iliyopita, wanadiplomasia waandamizi wa Marekani waliitembelea Sudan kwa lengo la kuimarisha jitihada zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa za kuwashawishi wanajeshi kurejesha utawala kamili wa kiraia nchini Sudan.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Volker Perthes mapema mwezi huu binafsi alianzisha mazungumzo na makundi mbalimbali ya Sudan katika harakati za kutafuta kuutatua mgogoro wa nchini humo.

Baraza linalotawala ambalo lililoundwa na jenerali Abdel Fattah al-Burhan baada ya mapinduzi na yeye mwenyewe kama mwenyekiti limepokea kwa furaha hatua ya mazungumzo ya Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo Marekani, Uingereza, Misri, Nchi za Falme za Kiarabu na Saudi Arabia pia zimefurahishwa na hatua ya Umoja wa Mataifa.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan
Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Kambi kuu ya kiraia inayopigania uhuru na mabadiliko nchini Sudan, pia ilijiunga kwenye mashauriano hayo kwa imani kwamba serikali ya mpito inayozingatia demokrasia itarejeshwa mamlakani.

Mamia ya wanaharakati wanaounga mkono demokrasia  wametiwa mbaroni nchini Sudan katika msako inayowalenga wanaharakati wa wanaopinga mapinduzi ya kijeshi. Mnamo siku ya Jumamosi, mwanaharakati mashuhuri anayetetea haki za wanawake, Amira Othman alikamatwa wakati vikosi vya usalama vilipovamia nyumba yake mjini Khartoum. Hayo ni kulingana na taarifa kutoka kwenye taasisi inayoendesha mpango wa kupinga ukandamizaji wa wanawake ambayo anaiongoza.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Volker Perthes amekosoa kukamatwa kwa Amira Othman, amesema kukamatwa kwa mwanaharakati huyo na unyanyasaji dhidi ya wanaharakati wanaotetea haki za wanawake unahatarisha na utapunguza pakubwa ushiriki wa wanawake katika siasa za nchini Sudan.

Chanzo: AFP/RTRE/AP