Moto umetumika kama silaha katika vita nchini Sudan
13 Mei 2024Shirika la haki za binadamu lenye makao yake nchini Uingereza la Sudan Witness limesema kuwa vijiji 72 na sehemu nyengine za maakazi ziliteketezwa moto mwezi uliopita na kufikisha idadi jumla ya makaazi yaliyoteketezwa moto nchini Sudan kuwa 201.
Mkurugenzi wa shirika hilo Anouk Theunissen ameeleza kuwa, hali ya moto kutumiwa kama silaha inatia wasiwasi na kwamba imesababisha mamia ya watu kuyakimbia makaazi yao.
Soma pia: Marekani yaonya uwezekano wa mauaji ya kimbari Sudan
Idadi ya matukio ya moto iliongezeka hasa maeneo ya kaskazini na magharibi mwa El-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini ambao unakabiliwa na wasiwasi wa kuzuka mapigano.
Kwa upande wake, mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Clementine Nkweta-Salami, ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti kwamba silaha nzito zinatumika katika mapigano katika mji wa El-Fasher nchini Sudan.