1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yakataa makubaliano na Sudan ya Kusini

24 Julai 2012

Sudan imekataa wazo la Sudan Kusini la kushusha gharama za kusafirisha mafuta ikisema kuwa ni lazima kwanza wasuluhishe masuala ya usalama baina yao katika wakati ambapo mapigano yanaripotiwa Darfur.

https://p.dw.com/p/15du2
Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan.
Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan.Picha: dapd

Hatua hiyo ya kutupilia mbali mpango huo uliopendekezwa na Sudan Kusini inachukuliwa wakati huu ambapo muda wa mwisho uliotolewa na Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika kwa nchi hizo kumaliza tofauti zake unakaribia kutumia.

Vyombo hivyo vilizipa Sudan na jirani yake muda wa hadi tarehe 2 mwezi Agosti kufukia makubaliano kuhusu malipo ya usafirishaji wa mafuta, mzozo wa mpaka na suala la usalama.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan na Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan ya Kusini.
Rais Omar al-Bashir wa Sudan na Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan ya Kusini.Picha: picture-alliance/dpa

Mpatanishi Mkuu kwenye mzozo huo kwa upande wa Sudan Kusini Pagan Amum, amewaambia waandishi wa habari kwamba nchi yake ilikuwa tayari kuanza tena shughuli za uchimbaji mafuta kufikia mwezi Januari mwakani kama gharama nafuu zingekubaliwa baina ya nchi hizo.

Sudan Kusini ilipendekeza kulipa kiasi cha dola za Marekani tisa kwa kila pipa moja la mafuta litakalosafirishwa kupitia Sudan, lakini nchi hiyo ikasema inataka dola 36 kwa kila pia ambayo inajumuisha shughuli za usafirishaji, kodi za bandari na usafishaji wa nishati hiyo.

Sudan: Amani kwanza biashara baadae

Sudan Kusini imesema kuwa kwa nia ya kulinda amani, ilikuwabali kumpa jirani yake huyo kiasi cha dola za Marekani bilioni 8.2 kwa kipindi cha miaka mitatu ambazo zinajumuisha fedha taslimu na misamaha ya madeni kusaidia kufidia pengo la uchumi ililolipata baada ya kutengana

Rais Salva Kiir Mayardit katika maadhimisho ya mwaka mmoja wa uhuru wa Sudan ya Kusini.
Rais Salva Kiir Mayardit katika maadhimisho ya mwaka mmoja wa uhuru wa Sudan ya Kusini.Picha: Reuters

Hata hivyo Sudan imetupilia mbali masuala yote hayo ikisema kuwa suala la usalama ndio jambo muhimu kwa sasa na kwamba taarifa za kuwa Sudan Kusini inawaunga mkono waasi ni lazima yapatiwe ufumbuzi.

Mjumbe wa jopo la wapatanishi kwenye mazungumzo baina ya nchi hizo kutoka Sudan Mutrif Siddiq, amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa Ethiopia kuwa umuhimu uwekwe kwenye masuala ya amani na usalama.

Hakuonyesha dalili ya kufikiwa kwa makubaliano yoyote kabla ya tarehe 2 Agasti lakini akasema kuwa ana matumaini na mambo yatakavyokwenda katika kipindi cha muda mrefu.

"Ni vigumu kupatikana suluhu katika kipindi cha siku 90 tu, baadhi ya mambo yanahitaji muda mrefu wa kuyajadili na kuyapatia muafaka" alisema Siddiq.

Mapigano Darfur

Wakati Sudan inakataa makubaliano ya kichumi na jirani yake, mapigano makali yameibuka kwenye jimbo la Darfur nchini humo baina ya waasi na vikosi vya serikali. Waasi wanasema kuwa wameliteka eneo la kambi ya jeshi pembezoni mwa Darfur linalopakana najimbo la Kusini la Kordofan.

Waasi wa Jeshi la Ukombozi wa Sudan jimboni Darfur.
Waasi wa Jeshi la Ukombozi wa Sudan jimboni Darfur.Picha: Reuters

Sudan inasema kuwa imewakamata wapiganaji kwenye eneo la Karkadi la Kordofan. Wapiganaji hao  ni wafuasi wa kundi la Justice and Equality Movement, JEM, ambalo lina makao yake jimboni Darfur. Mazungumzo baina ya pande hizo yalianza kwenda vibaya mwishoni mwa wiki mjini Addis Ababa.

Mwandishi: Stumai George/DPAE/AFPE/Reuters
Mhariri: Josephat Charo