1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sunak akwama tena bungeni kupeleka wakimbizi Rwanda

18 Aprili 2024

Baraza la juu la bunge la Uingereza limekataa kwa mara ya nne sheria ya kuwezesha mpango wa Waziri Mkuu Rishi Sunak kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda.

https://p.dw.com/p/4ev3T
 Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak, amekwama tena bungeni kwenye juhudi zake za kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda.Picha: Benjamin Cremel/Pool via REUTERS

Sheria hiyo inaonekana na serikali kuwa muhimu ili kuondokana na vikwazo vya kisheria vilivyopo kwenye mpango huo, ambao serikali inataka kuanza kuwapeleka Rwanda waomba hifadhi wanaofika kinyume cha sheria nchini Uingereza.

Hata hivyo, mabaraza yote mawili ya bunge la Uingereza lazima yaafiki maneno yaliyotumika kwenye mswada huo kabla ya kuwa sheria.

Soma zaidi: Uingereza, Rwanda zatarajia kuwahamisha wahamiaji wiki chache zijazo

Siku ya Jumatano (Aprili 17), baraza la juu lilipiga kura ya kuunga mkono kufanya mabadiliko sheria iliyoidhinishwa na baraza la chini la bunge.

Waziri wa Mambo ya Ndani, James Cleverly, aliukosoa upinzani wa chama cha Labour, ambacho wabunge wake walipiga kura kuipinga serikali.