1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sweden kulimana na Uhispania nusu fainali

14 Agosti 2023

Katika tamasha la Kombe la Dunia la Wanawake linaloendelea Australia na New Zealand ambalo sasa limefika hatua ya nusu fainali na wa kwanza kujitosa dimbani katika mchezo wa kwanza Jumanne ni Sweden na Uhispania

https://p.dw.com/p/4V8l8
Frauen-WM-Viertelfinale | Japan gegen Schweden
Sweden hawajawahi kubeba Kombe la Dunia la WanawakePicha: Abbie Parr/AP/picture alliance

Sweden walimaliza nafasi ya pili katika Kombe la Dunia 2003 na wamemaliza wa tatu mara tatu, lakini hawajawahi kushinda kombe hilo kubwa Zaidi la kandanda. Sweden na Uhispania hazijawahi kukutana katika Kombe la Dunia. Kocha wa Sweden Peter Gerhardsson anawachambua wapinzani wao

Lakini kitu kizuri ni wakati wanapoupoteza mpira, wanakuwa wepesi sana. Ni wazuri katika kuuchukua tena kwa hiyo tunapaswa kuwa bora zaidi katika kuusambaza mpira kuliko tulivyokuwa dhidi ya Japan. na kwa sababu walijilinda zaidi kuliko tulivyodhani, sidhani hivyo ndivyo itakavyokuwa mechi ya kesho

Frauen Fußball WM
Uhispania hawataka kuweka historia kufika fainaliPicha: Cameron McIntosh/Xinhua News Agency/picture alliance

Kocha wa Uhispania Jorge Vilda amesema timu yake isingekuwa katika nusu fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake kama shirikisho la kandanda la nchi yake halingemuunga mkono wakati wa uasi uliofanywa na wachezaji mwaka jana. Karibu wachezaji 15 walitishia kujiondoa kikosini kama kocha aliyehudumu kwa muda mrefu Vilda asingefutwa kazi. Mkuu wa chama cha soka Uhispania akamuunga mkono Vilda ambaye aliwafungia nje ya kikosi baadhi ya wachezaji waliaosi kabla ya kuwakaribisha baadhi yao kwa ajili ya Kombe la Dunia. Kocha Vilda anasema hayo yamepita na sasa wana kazi ya kuandikisha historia "Nahisi Sweden huenda wana wajibu wa kutupiga kwa sababu ya rekodi yao ya kihistoria. Lakini pia nna uhakika kuhusu mchezo wetu, na hivyo ndivyo nnavyoona, kwamba tunaweza kuwatizama usoni na kuonyesha Uhispania iliyo bora zaidi na kushinda mechi ya kesho."

Hii ni mara ya tatu kwa Uhispania kucheza katika mashindano haya na ni mara ya kwanza kutinga nusu fainali. 

Australia kuvaana na England

Kombobild Flaggen Australien und England
Asutralia na England ni watani wa jadi kimichezo

Katika nusu fainali ya pili Australia watashuka dimbani dhidi ya England Jumatano mjini Sydney. Ni mechi yenye uhasama wa muda mrefu wa michezo kati ya nchi hizo. Wenyeji wenza Australia wana taifa zima nyuma yao wakati wakicheza mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Dunia katika historia yao na mashabiki 80,000 wanatarajiwa kumiminika uwanjani.

England ndio mabingwa wa Ulaya na wanapigiwa upatu kutinga fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza. Kocha wa England Mholanzi Sarina Wiegman atakuwa bila ya huduma za Lauren James ambaye alifungiwa mechi mbili. Naye kocha wa Australia Tony Gustavsson anahitaji kufanya uamuzi kama ataanza mechi na nahodha wake Sam Kerr katika safu ya ushambuliaji.

afp, ap, dpa