Sweden yaishutumu Iran kuhusika na ujumbe wa kulipiza kisasi
24 Septemba 2024Mamlaka nchini Sweden, leo imeishtumu Iran kwa kuhusika na kutumwa kwa maelfu ya ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi kwa watu nchini humo kuwataka kulipiza kisasi kuhusiana na kuchomwa kwa kitabu kitakatifu cha Qur'an mwaka 2023.
Maafisa mjini Stockholm walidai kuwa kikosi cha ulinzi wa mapinduzi ya Iran IRGC, kilifanya udukuzi wa data na kutuma ujumbe 15,000 wa maandishi kwa lugha ya Kiswidi kuhusiana na msururu wa uchomaji wa umma wa Qur'an.
Mwendesha mkuu wa mashtaka Mats Ljungqvist, amesema uchunguzi wa awali uliofanywa na taasisi ya usalama wa ndani wa Sweden SAPO, ulionesha kuwa ni serikali ya Iran iliyofanya udukuzi huo wa data kupitia kikosi hicho cha IRGC, katika kampuni moja ya Sweden inayoendesha huduma kubwa ya mawasiliano ya ujumbe mfupi.
Shirika la habari la Sweden SVT, lilichapisha picha ya ujumbe huo uliosema'' "wale walioivunjia heshima Qur'an lazima kazi zao zifunikwe kwenye majivu" na kuwaita raia wa Sweden ''ibilisi''.