Syria kutekeleza matakwa ya jumuiya za kiarabu au iwekewe vikwazo
25 Novemba 2011Wanaharakati hao wamewataka raia wote nchini Syria kuandamana baada ya Sala ya ijumaa kuunga mkono wanajeshi walioasi, wakisema kuwa wanajeshi hao wanawalinda kutokana na ghasia zinazosababishwa na wanajeshi waliowatiifu kwa serikali.
Waandamanaji nchini Syria wamekuwa wakiandamana kutaka demokrasia na utwala mpya tangu miezi nane iliopita. "Jeshi hili lililoasi ndilo linalotulinda katika mageuzi yetu ya amani, wanajeshi waliowatiifu kwa serikali wamekuwa wakitekeleza mauaji kila siku" alisema mmoja wa wanaharakati hao.
Kulingana na shirika la kutetea haki za kibinaadam nchini Syria Watu 51 waliuwawa hapo jana wakiwemo wanajeshi 23.
Uamuzi wa jumiya ya nchi za kiarabu kwa Syria kutaka wakubali waangalizi wa kimataifa kuingia nchini humo la sivyo kuwekewa vikwazo imekuja baada ya kumalizika kwa kikao cha mawaziri wa mambo ya kigeni mjini Cairo ambapo mawaziri hao 22 kwa mara ya kwanza walimuomba mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon kuingilia kati katika kusuluhisha mzozo unaoendelea nchini Syria.
Hata hivyo Urusi imelaani tukio la kuwekewa vikwazo Syria na kusema hatua ya kusuluhisha mambo ni kupitia mazungumzo na sio kuwekewa Vikwazo. Iwapo Syria itashindwa kutia saini mkataba wa kuwaruhusu waangalizi wa kimataifa wakiwemo waandishi habari kuingia nchini humo, mawaziri wa fedha watakutana siku ya jumamosi kupiga kura na kuamua ni vikwazo gani vinapaswa kuwekwa dhidi ya Syria, ikijumuishwa kufutiliwa mbali safari za ndege huko na kuzuiwa kwa fedha za serikali.
Hata hivyo maafisa pamoja na wanaharakati nchini nchini Syria wamesema iwapo jumuiya ya nchi za kiarabu itawawekea vikwazo, hali hiyo itawadidimiza kiuchumi.
Waziri wa uchumi Mohammed Nidal al-Shaar amesema Syria inategemea pakubwa mataifa ya kiarabu katika bishara zake, Mohammed amesema ana hakika kuwa sio mataifa yote ya kiarabu yatapiga kura dhidi ya Syria, amesema tayari Lebanon imetoa hakikisho la kuwaunga mkono.
Lebanon na Yemen walikuwa wa kwanza kupinga hatua ya jumuiya hiyo kuiondoa kwa muda Syria katika uanachama wake. "Sidhani kama Iraq itapiga kura ya kutuwekea vikwazo" alisema afisa mmoja wa serikali nchini Syria ambaye ni mshirika wa karibu wa waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki.
Umoja wa mataifa umesema kuwa watu elfu 3,500 wameuwawa wengi wao wakiwa ni raia tangu kuanza kwa wimbi la mapinduzi tarehe 15 mwezi machi mwaka huu, huku maelfu ya waandamanaji wakizuiliwa.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdulrahman