Syria: Wakaazi wa jimbo la Idlib bado wana wasiwasi mkubwa
20 Septemba 2018Miaka saba baada ya vita vya nchini Syria majeshi ya nchi hiyo na washirika wao wa Urusi walikuwa wamepanga kulikomboa jimbo la Idlib ambalo ni ngome ya mwisho ya waasi wa nchini Syria. Raia kati ya milioni tatu hadi nne wanaishi katika jimbo hilo. Lakini hakuna mwenye uhakika juu ya hesabu hizo. Karibu nusu ni wale walioyakimbia majimbo mengine ya Syria. Kwa watu hao jimbo la Idilib la kaskazini magharibi mwa Syria ndiyo matumaini yao ya mwisho.
Familia nyingi zilizokimbilia kwenye mpaka na Uturuki zina wasi wasi juu ya ndugu na jamaa zao. Raia mmoja Abdulmajid Al-Halabi huwasiliana na dada yake Fatima kwa njia ya Whatsapp wakati huduma za mtandao wa Intaneti zikiwepo. Fatima hakutarajia kuona vita vya nchini Syria vikiendelea. Miaka sita iliyopita alikimbillia kwenye mpaka na Uturuki. Hata hivyo, hali sasa imebadilika baada ya Uturuki kuufunga mpaka wake na Syria na imejenga uzio wa kilometa 800 kwa lengo la kuwazuia magaidi na wahalifu wanaosafirisha binadamu kinyume cha sheria.
Wakimbizi wa Syria zaidi ya milioni tatu na nusu wanaishi nchini Uturuki. Rais Recep Tayyip Erdogan hivi karibuni alisema kuwa nchi yake imefikia mwisho wauwezo wake katika kuwapokea wakimbizi wa Syria. Shida za wakimbizi hao zinaongezeka. Kutokana na hofu ya mashambulio ya majeshi ya Syria na washirika wake wa Urusi maalfu ya wakimbizi wa Syria wamekimbilia karibu na mpaka wa Uturuki.
Kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya misaada wakimbizi wa Syria zaidi ya laki saba wamelundikana karibu na mpaka wa Uturuki. Afisa mmoja wa shirika la misaada Kadir Akgündüz amesema watu hao wanaishi kwa dhiki. Hata hivyo afisa huyo amesema makubaliano yaliyofikiwa baina ya Urusi na Uturuki ya kuahirisha mashambulio ni hatua ya mafanikio.
Viongozi wa nchi hizo marais Putin na Edogan walikubaliana mwanzoni mwa wiki, kujenga ukanda wa usalama katika jimbo la Idlib hadi ifikapo tarehe 15 mwezi ujao. Ukanda huo utasimamiwa na wanajeshi wa Uturuki na polisi ya Syria na jeshi la Urusi. Kulingana na makubaliano kati ya marais wa Urusi na Uturuki, wapiganaji wenye itikadi kali na hasa wa kundi la kigaidi la Al-Nusra watapaswa kuondoka Idlib.
Lakini haijafahamika jinsi zoezi hilo litakavyotekelezwa. Hata hivyo, Rais Erdogan wa Uturuki amesema makubaliano yaliyofikiwa ni mafanikio ya kidiplomasia. Amesema Uturuki na Urusi zimeweza kuepusha maafa makubwa kwa binadamu katika jimbo la Idlib. Baadhi ya wakimbizi wa Syria walioko kwenye mpaka na Uturuki wamesema hata hivyo makubaliano hayo hayana maana ya kumalizika haraka kwa vita vya nchini Syria.
Mwandishi: Zainab Aziz/Hahn Julia
Mhariri: Mohammed Khelef