Syria yafanya maziko ya wahanga wa shambulizi la droni
6 Oktoba 2023Shambulio hilo la jana Alhamisi lilifanyika mara baada ya kumalizika kwa mahafali ya maafisa wa kijeshi, na liliuwa na kujeruhi maafisa wa kijeshi pamoja na familia zao.
Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti leo Ijumaa kwambawatu 89 waliuawa, lakini shirika la ufuatiliaji wa haki za binadamu la Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza, limesema watu 123 waliuawa, wakiwemo raia 54, 39 kati yao wakiwa wanawake na watoto.
Limeongeza kuwa watu wasiopungua 150 walijeruhiwa, Waziri wa ulinzi wa Syria Ali Mahmoud Abbas amehudhuria maziko ya kwanza ya takribani watu 30.
Katika maeziko hayo amesema heshima na ustawi wa taifa vina thamani kubwa, na thamani kubwa zaidi ambayo mtu anaweza kulipa kwa taifa lake ni kutoa uhai wake.
"Kwa wale mashahidi waliotoa maisha yao kwa ajili ya taifa, bila shaka damu yao ni ya thamani sana" Alisema Mahmoud
Aliongeza kwamba kila raia anayo nafasi ya kupigania maslahi ya taifa na kupiga vita uhalifu wa kila namna.
Makundi ya kigaidi yanahusika katika shambulio?
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo mpaka sasa, lakiji jeshi la Syria hapo jana lilituhumu kile lilichokiita "makundi ya kigaidi" kuhusika na shambulio hilo lililofanywa na droni zilizofungiwa vilipuzi, na kuapa kujibu kwa nguvu kamili.
Picha za vidio zinazosambaa kwenye mitandao ya Kijamii zinaonyesha taharuki na machafuko kwenye chuokilicholengwa, huku watu wakianguka chini na wengine wakiomba msaada.
Katika mkoa wa Idlib ambao ni ngome ya mwisho ya waasi wa upinzani kaskazini-magharibi mwa Syria, wakaazi wameripoti mashambulizi makubwa ya vikosi vya serikali, katika kile kinachodhihirika kuwa ulipaji kisasi, ambapo raia 15 wameripotiwa kuuawa.
Maeneo makubwa ya mkoa wa Idlib na maeneo yanayopakana na mikoa ya Aleppo, Hama na Latakia yanadhibitiwa na kundi la wapiganaji la Hayati Tahrir al-Sham, linaloongozwa na tawi la zamani la kundi la Al-Qaeda nchini Syria.
Soma pia:Umoja wa Mataifa bado unahimiza suluhu ya amani nchini Syria na kutaka kukomeshwa ghasia
Kundi hilo la jihadi limetumia droni kushambulia maeneo yanayodhibitiwa na serikali huko nyuma.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alielezea wasiwasi mkubwa kuhusiana na mashambulizi hayo pamoja na mashambulizi ya kujibu ya jeshi la Syria, kulingana na msemaji wake Stephane Dijarric.
Rais wa Urusi Vladmir Putin amemtumia salaam za rambirambi mwenzake wa Syria Bashar al-Assad kufuatia shambulio hilo.
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria, Geir Pedersen, amesema katika taarifa kuwa shambulio hilo la jana, linalotajwa kuwa baya kabisaa katika vita vya miaka 12 nchini Syria, ni ukumbushi wa haja ya kupunguza haraka vurugu, kuelekea usitaji wa mapigano nchini humo, na mkakati wa ushirikiano wa kukabiliana na makundi ya kigaidi yalioorodheshwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Syria imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia leo Ijumaa.