Syria yakanusha madai kuhusu silaha za kemikali
28 Aprili 2013"Kwanza ya yote napenda kuthibitisha kuwa taarifa zilizotolewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani na serikali ya Uingereza hazina ukweli wowote na ni uongo ulio dhahiri," alisema waziri wa habari Omran al-Zohbi katika mahojiano yaliyochapishwa na tovuti ya Russia Today, inayofadhiliwa na ikulu ya Urusi, Kremlin. "Nataka kusisitiza mara nyingine tena kwamba Syria kamwe haiwezi kuzitumia silaha hizo, sio tu kwa kuheshimu sheria za kimataifa na sheria za kuongoza vita, lakini kutokana na sababu za kibinaadamu na maadili," alisema Zohbi.
Wapinzani wasisitiza kemikali zimetumika
Lakini muungano mkuu wa upinzani umepinga makanusho hayo, na kuwanukuu waasi mjini Daraya, karibu na Damascus wakisema makombora yaliyobeba vichwa vyenye gesi ya sumu yaliripuriwa siku za Alhamisi na Ijumaa dhidi ya mji huo. Yaliporipuka, "yalisababisha wingu kubwa la gesi. Miripuko hiyo ilipelekea kiasi ya 42 kukosa pumzi, kuzimia na kutapika," ilisema taarifa. Muungano huo umetaka kufanyike uchunguzi wa kimataifa katika madai ya mashambulizi hayo.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameutaka utawala mjini Damascus kuruhusu wakaguzi wa umoja huo kuchunguza madai ya matumizi ya silaha za kemikali katika mogogoro huo unaosambaa, ambao uliripuka Machi 2011. Lakini Zohbi alisema Syria haiwezi kuwaamini wakaguzi wa umoja wa mataifa kutoka Uingereza na Marekani. "Pia hatuna imani na sifa zao, lengo lao ni kuchezea ukweli," aliiambia Russia Today. "Hatutajali kama Warusi watakuwa miongoni mwa wakaguzi, kinyume na hivyo, tunakaribisha tu wazo hili. Tuna uhakika na sifa zao na uwezo wao katika mambo kama haya," alinukuliwa akisema Zohbi.
Pamoja na China, Urusi imetilia guu maazimio kadhaa ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, yanayotishia vikwazo dhidi ya serikali ya rais Bashar al-Assad. Rais wa Marekani Barack Obama aliionya Syria siku ya Ijumaa, kuwa matumizi ya silaha za kemikali yatakuwa "jambo litakalobadilisha mchezo mzima", baada ya Marekani, Israel na Uingereza kuonyesha dalili kuwa utawala wa Assad ulitumia kemikali hatari ya sarin.
Utawala wa Obama wachukuwa tahadhari
Lakini Obama alisema Washington lazima ithibitishe kikamilifu, vipi na lini silaha hizo zilitumika, akiahidi uchunguzi kamili wa Marekani na kimataifa katika ripoti za hivi karibuni. Urusi imeonya dhidi ya kutumia ripoti hizi kuingilia kijeshi nchini Syria. "Lazima tuhakiki taarifa hizi mara moja na kufuata vigezo vya kimataifa, na tusizitumie kutimiza malengo mengine. Hazipaswi kuwa kisingizio cha kuiingilia kijeshi Syria," alisema naibu waziri wa mambo ya kijegi wa Urusi Mikhail Bogdanov mjini Beirut.
Zohbi alihusisha shutuma za matumizi ya silaha za kemikali kwa kile alichosema ni "mabadiliko yaliyofanywa katika uwanja wa kivita" ambayo yamevinufaisha vikosi vya serikali, limeripoti shirika la habari la RIA Novosti. Siku ya Ijumaa katika matamshi yaliyochapishwa na shirika la habari la Interfax, kuwa silaha za kemikali zilitumia na waasi na zilitolewa nchini Uturuki.
Upinzani wa Syria umeongeza shinikizo kwa kulitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za mara moja, ikiwezekana hata kuweka eneo lisiloruhusiwa kuruka ndege kwa Syria. Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, alisema ushahidi unaozidi kwamba Assad alitumia kemikali dhidi ya watu wake ulikuwa "mzito sana."
Mapigano yaendelea kwa kasi ileile
Siku ya Jumamosi mapigano yaliendelea kwa nguvu ileile, ambapo watu wasiopungua 32 waliuawa nchini kote, wakiwemo 10 katika mashambulizi dhidi ya mji wa Douma, Kaskazini-Mashariki mwa Damascus, lilisema shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria. Shirika hilo pia liliripoti kuwa waasi waliiteka kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Handarat katika kingo za Aleppo, baada ya miezi kadhaa ya mapigano makali.
Wachambuzi wanasema majirani wa Syria wanakabiliwa na hatari inayozidi ya mgogoro huo kusambaa katika kanda, wakati ambapo Assad akiwa tayari kufanya lolote ili kuwasimamisha waasi. Wanasema Lebanon na Jordan ndiyo ziko katika hatari zaidi, huku Iraq huenda nayo ikaathirika huko mbeleni, pamoja na Israel na uturuki. "Ni kanda iliyoko katika hatari kubwa, na kuna hatari ya kuongezeka," alisema Anthony Skinner, kutoka shirika la ushauri la Uingereza Maplecoft.
Waziri mkuu wa Iraq Nuri al-Malik, akiitaja kwa juuju Syria, alisema machafuko yanayoongezeka nchini mwake yalirudi Iraq "kwa sababu yalianzia katika eneo lingine ndani ya kanda hiyo." Wakati huo huo, maafisa wa ngazi za juu nchini Misri waliitembelea Iran kujadili pendekezo la mataifa manne ya Kiilsamu ya Misri, Uturuki, Saudi Arabia na Iran, kusaidia kutatua mgogoro wa Syria, ilisema ofisi ya rais wa Misri.
Cairo, Ankara na Riyadh zinaunga mkono waasi ambao kiasi kikubwa ni wasunni nchini Syria, wakati Iran inaoyoongozwa na Washia, inaunga mkono utawala wa Assad unaoongozwa na kabila la wachache la Alawi.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Amina Abubakar