Syria:Mashambulizi ya magharibi yakiuka sheria za kimataifa
14 Aprili 2018
Serikali ya Syria imeyaita mashambulizi ya mataifa ya magharibi kwenye mitambo yake ya kijeshi, kuwa ya kikatili na kijinga na kwamba yamekiuka sheria za kimataifa. Marekani, Ufaransa na Uingereza zimefanya mfululizo wa mashambulizi ya angani Jumamosi asubuhi katika maeneo ya karibu na mji mkuu wa Damascus na katikati mwa mji wa Homs.
Operesheni hiyo ya pamoja inakuja wiki moja baada ya shambulizi la kemikali linalodiawa kufanywa kwenye mji unaodhibitiwa na waasi nje kidogo ya Damascus na kuwaua watu 40. Mataifa ya magharibi yalimtuhumu rais Bashar al Assad kwa shambulizi hilo, lakini Syria na mshirika wake Urusi wamekana madai hayo na kuyatuhumu mataifa hayo kwa kutengeneza tukio hilo ili kuhalalisha hatua za kijeshi.
Kundi la Hezbollah la nchini Lebanon, mshirika wa serikali ya Syria, limelaani mashambulizi hayo na kusema mataifa hayo hayatatimiza malengo yake.
Miripuko ilionekana ikitoa mwanga katika anga la mjini wa Damascus, mji mkuu wa Syria, wakati Trump akizungumza kutokea Ikulu ya White House.
Televisheni ya Syria imeripoti kwamba vifaa vya ulinzi wa anga nchini Syria , ambao ni muhimu , vilijibu shambulio hilo. Baada ya shambulio kusita na hali kutulia, magari yakiwa na vipaza sauti yaliingia mitaani katika mji mkuu Damscus yakipiga muziki wa kauli mbiu za kitaifa.
Trump alisema Marekani iko tayari kuendelea na mbinyo dhidi ya Assad hadi pale atakapofikisha mwisho kile rais huyo alichosema utaratibu wake wa kihalifu wa kuwauwa raia wake kwa silaha za sumu zilizopigwa marufuku kimataifa. Haijafahamika mara moja iwapo Trump alikuwa na maana kwamba operesheni hiyo ya kijeshi ya washirika itaendelea zaidi ya mashambulio hayo ya awali ya makombora.
"Shambulio la uovu na la kinyama limesababisha wakina mama na baba , watoto wachanga na vijana , wakitapia maisha yao kwa kukosa hewa. Haya si matendo ya kibinadamu , badala yake ni uhalifu wa zimwi," alisema Trump.
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May alisema mjini London kwamba mataifa ya magharibi yamejaribu "kila kinachowezekana" kwa njia ya kidiplomasia kumzuwia Assad dhidi ya kutumia silaha za sumu. "Lakini juhudi zetu kila mara zimezuiwa" na Syria na Urusi, amesema.
Kubadili utawala
"Kwa hiyo hakuna nafasi mbadala ila kutumia nguvu kuharibu na kuizuwia serikali ya Syria kutumia ya silaha za sumu," May alisema.
"Hii haihusiani na kuingilia kati katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Haihusiani na kubadilisha utawala."
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema katika taarifa kwamba lengo la shambulio hilo lilikuwa hazina ya silaha za sumu iliyofichwa na serikali ya Syria."
Trump hakutoa maelezo juu ya shambulio hilo la pamoja la Marekani, Uingereza na Ufaransa, lakini ilikuwa inatarajiwa kujumuisha makombora kadhaa yaliyorushwa kutoka nje ya anga la Syria. Amefafanua lengo kuu kuwa ni kuonesha upinzani mkubwa dhidi ya matumizi ya silaha za sumu.
Serikali ya Syria imekana mara kadhaa kutumia silaha zilizopigwa marufuku.
Stoltenberg aunga mkono shambulio
Uamuzi wa kushambulio , baada ya siku kadhaa za majadiliano, ni hatua ya pili ya Trump kuamuru shambulio nchini Syria.
Aliamuru kushambuliwa kwa kituo cha kijeshi nchini Syria mwezi Aprili 2017 kwa makombora kadhaa chapa Tomahawk kwa kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Assad kutumia gesi ya sarin dhidi ya raia.
Katibu mkuu wa jumuiya ya NATO Jens Stoltenberg ameelezea kuunga kwake mkono mashambulizi ya anga ya mataifa ya magharibi nchini Syria leo Jumamosi baada ya shambulio lililolenga utawala wa Bashar al-Assad ikiwa ni jibu kwa shambulio linaloshukiwa kufanywa na utawala huo la silaha za sumu. Naunga mkono shambulio lililofanywa na Marekani, Uingereza na Ufaransa , hii itapunguza uwezo wa utawala wa Syria kuwashambulia zaidi watu wake kwa silaha za sumu," amesema Stoltenberg.
Katika wizara ya ulinzi ya Marekani , waziri wa ulinzi Jim Mattis alisema shambulio hilo lilikuwa kubwa dhidi ya serikali ya Syria kuliko ilivyokuwa mwaka 2017 na lililenga miundo mbinu ya silaha za sumu nchini Syria. Alilieleza shambulio hilo kuwa ni "pigo moja," na kuongeza, "Naamini limefikisha ujumbe mzito."
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Isaac Gamba