1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yapongeza uamuzi wa Urusi, Iran na Uturuki

23 Novemba 2017

Serikali ya Syria imeupongeza uamuzi uliofikiwa kati ya marais wa nchi washirika wake Urusi na Iran pamoja na Uturuki inayowaunga mkono waasi, wa kufanyika kwa mazungumzo ya amani kati ya serikali na vikosi vya waasi.

https://p.dw.com/p/2o9GM
Syrien Präsident Assad - Rede vor Diplomaten in Damaskus
Picha: picture-alliance/AP Photo/Syrian Presidency

Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Syria imesema kuwa nchi hiyo inapongeza kufikiwa kwa makubaliano hayo kwa sababu siku zote Syria inaunga mkono juhudi zozote zile za kisiasa ambazo zinaheshimu uhuru na uadilifu na katika kusaidia kumaliza umwagikaji wa damu nchini Syria.

Rais wa Urusi, Vladmir Putin, alisema jana katika mkutano uliofanyika Sochi, Urusi kwamba marais wenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na Iran, Hassan Rouhani wamekubaliana kuwepo kwa mkutano ambao umepangwa kufanyika mjini Geneva, Uswisi wiki ijayo.

Putin amesema awamu mpya ya mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, itawakutanisha pamoja Rais wa Syria, Bashar al-Assad, wawakilishi kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa pamoja na makundi ya upinzani ya ndani na nje ya Syria kwa lengo la kujadiliana mustakabali wa Syria na kuhakikisha unapatikana ufumbuzi wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka sita.

Sochi Treffen mit Erdogan, Putin und Rohani
Viongozi wa Uturuki, Urusi na Iran wakiwa kwenye mkutano SochiPicha: picture-alliance/dpa/M.Metzel

Hata hivyo, Erdogan anaonekana kukasirishwa na uwezekano wa kualikwa katika mkutano huo wa amani kundi la Kikurdi la PYD na vikosi vya ulinzi wa Wakurdi, YPG ambavyo vinapigana nchini Syria. Erdogan bila ya kuyataja majina, amesema katika mkutano wa Sochi kwamba hawawezi kufikiria kuyaalika makundi ya kigaidi katika mkutano huo, kama wajumbe halali.

''Kuondokana na magaidi wanaotishia umoja wa kisiasa wa Syria, uadilifu pamoja na usalama, kitaendelea kuwa kipaumbele chetu. Mtu yeyote asitegemee tukae pamoja na makundi ya kigaidi yanayotishia usalama wa taifa letu,'' alisema Erdogan.

Jitihada zimekwama kwa mara kadhaa

Juhudi kadhaa za kumaliza vita nchini Syria zimekwama, huku kizingiti kikubwa kikiwa kuhusu hatma ya Rais Assad, ambaye wapinzani wanamtaka aondoke madarakani mara moja. Urusi, Uturuki na Iran zinashirikiana kwa pamoja katika kuongeza nguvu ya kumaliza vita vya Syria, ingawa Uturuki inawaunga mkono waasi, kinyume ilivyo kwa Urusi na Iran.

Saudi Arabien politische Beratungen der syrischen Opposition in Riad
Wajumbe waliohudhuria mkutano wa upinzani wa Syria mjini RiyadhPicha: Getty Images/AFP/F. Nureldine

Kundi kubwa la upinzani nchini Syria linalokutana mjini Riyadh, Saudi Arabia, limesisitiza leo kuwa Assad asipewe jukumu lolote katika mazungumzo hayo ya amani, licha ya uvumi kwamba hatua hiyo inaweza kurahisisha msimamo wake kuelekea katika kipindi cha mpito wa kisiasa. Taarifa hiyo imetolewa mwishoni mwa mkutano wao.

Wakati huo huo, vikosi vya Iraq leo vimeanzisha operesheni ya kulisafisha eneo la mpaka kati ya Syria na Iraq, kwa lengo la kuwaondoa wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Taarifa ya jeshi la Iraq imesema kuwa majeshi ya Iraq pamoja na vikosi vya wapiganaji wa Kishia PMF, wanashiriki katika operesheni hiyo dhidi ya wanamgambo waliojificha kwenye msitu wa eneo hilo la mpakani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef