Syria yarejea katika Umoja wa kiarabu
7 Mei 2023Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa nchi za kiarabu wameamua kuirejesha Syria kwenye jumuiya hiyo baada ya nchi hiyo kusimamishwa uanachama kwa muda wa zaidi ya mwongo mmoja. Hatua hiyo inaimarisha juhudi za jumuiya hiyo za kusawazisha uhusiano na rais Bashar al-Assad. Msemaji wa katibu mkuu wa kundi la nchi hizo ameeleza kuwa uamuzi huo ulipitishwa kwenye mkutano wa faragha uliofanyika mjini Cairo, makao makuu ya umoja wa nchi za kiarabu. Syria ilisimamishwa uanachama mnamo mwaka 2011 baada ya serikali ya Assad kutumia mabavu kukabili maandamano dhidi ya rais huyo yaliyosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hivi karibuni nchi kadhaa za kiarabu pamoja na Saudi Arabia zilianzisha tena mikutano na ziara za ngazi za juu na Syria. Nchi za kiarabu zinajaribu kufikia uamuzi wa pamoja juu ya kumwalika rais Assad kwenye mkutano wao wa kilele unaotarajiwa kufanyika mjini Riyadh,Saudi Arabia, wiki mbili zijazo.