Taarifa mchanganyiko Ukraine tangu uvamizi wa Urusi
20 Aprili 2023Urusi imeishambulia Ukraine kwa zaidi ya dazeni mbili za ndege zisizo na rubani katika saa 24 zilizopita hayo ni kwa mujibu wa taarifa za jeshi la Ukraine. Hata hivyo mfumo wa ulinzi wa anga wa Ukraine uliweza kuziangusha ndege 21 kati ya 26 zisizo na rubani aina ya Shahed-136. Aidha, taarifa ya jeshi la Ukraine imesema wanajeshi wake wamehimili kwa mafanikio mashambulizi 55 ya ardhini ya Urusi katika mapigano yanayoendelea huko mashariki mwa mkoa wa Donetsk, ambapo unapatikana mji unaoshindaniwa vikali wa Bakhmut.
Wakati huohuo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kijeshi ya NATO, Jens Stoltenberg anaitembelea Ukraine kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo ilipovamiwa na Urusi hapo mwaka jana. Stoltenberg amesisitiza ahadi za muungano wa kijeshi wa NATO katika kutetea uhuru wa Ukraine.
Soma: Zelensky, Putin wayatembelea maeneo ya vita nchini Ukraine
Kuhusu mwangaza mkali kwenye anga ya jiji la Kiyv uliosababisha hofu kubwa kwa wakaazi wa jiji hilo, waliodhani huenda lingefuata shambulio la makombora ya Urusi, naibu mkuu wa udhibiti katika wakala wa kitaifa wa anga za juu nchini Ukraine, Igor Korniyenko aliwatowa watu wasiwasi kwa kusema ingawa idara yake haikuweza kutambua mara moja mwanga huo mkali ulikuwa ni kitu gani lakini wanadhani ulikuwa ni kimondo. Lakini jeshi la Ukraine limetangaza kupitia mtandao wa Telegram kwamba mwanga huo unaweza kuwa ulisababishwa na satelaiti ya zamani ya NASA iliyoingia kwenye anga ya dunia.
Kwingineko Denmark na Uholanzi zimesema zitanunua vifaru 14 vya Leopard 2 na kuvipeleka Ukraine, wakati nchi hiyo ikiahidiwa kuongezewa silaha nzito. Taarifa ya nchi hizo mbili imesema vifaru hivyo vitawasilishwa kwa Ukraine mapema mwaka ujao, 2024 na kwamba makadirio ya gharama ya ununuzi wake ni euro milioni 165 zitakazotolewa sawa kwa sawa na Denmark na Uholanzi.
Soma:Urusi yaushambulia mkoa wa Odesa kwa ndege za Drone
Na ukaguzi ndani ya meli za nafaka zinazohudumu kwenye Bahari Nyeusi ulianza tena Jumatano baada ya kusimama kwa muda kutokana na pande zinazohusika kuhitaji muda zaidi ili kukubaliana juu yavipaumbele vya uendeshaji wa mpango huo.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Ismini Palla, anayesimamia mpango huo, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba meli zote zinazoingia na kuondoka kutoka Ukraine zimekaguliwa na maafisa kutoka Urusi, Ukraine na Uturuki kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa. Palla amesema pande zote zimekubaliana juu ya orodha ya meli zinazotakiwa kuhudumu.
Vyanzo: DPA/AP/AFP/RTRE