Watu 28 wauawa kutokana na maporomoko ya ardhi Cameroon
10 Oktoba 2023Kulingana na shirika la habari la CRTV nchini humo, maporomoko ya ardhi katika wilaya ya Mbankolo Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo, yalisababisha kusombwa kwa takriban nyumba 30. Waokoaji wanasema kufikia sasa, wamepata miili 23 katika matope na vifusi lakini wakaonya kuwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka huku shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea.
Maporomoko ya ardhi hutokea mara kwa mara
Maporomoko hayo ya ardhi ni ya kawaida mjini Yaounde wakati wa msimu wa mvua. Mamlaka inasema kuwa nyumba nyingi zilizosombwa zilikuwa zimepangiwa kubomolewa kutokana na ujenzi duni.
Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, watu wasiopungua 15 waliuawa katika maporomoko ya ardhi katika jiji hilo.
Mwaka wa 2019, watu wapatao 43 waliuawa katika tukio kama hilo katika mji wa Magharibi wa Bafoussam.