Bwawa laporomoka Sudan na kusababisha vifo vya watu 30
27 Agosti 2024Ukinukuu mamlaka za eneo hilo, Umoja huo wa Mataifa umesema makazi ya takriban watu 50,000 yaliathirika kutokana na mafuriko hayo na kwamba idadi hiyo ni ya eneo la magharibi mwa bwawa hilo la Arbaat kwasababu eneo la mashariki haliwezi kufikiwa.
Bwawa hilo la Arbaat liko umbali wa kilomita 40 tu kaskazini mwa Port Sudan, eneo lenye majengo ya serikali, wanadiplomasia, mashirika ya misaada na makazi ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao.
Mabomba ya umeme na maji yameharibiwa
Katika ujumbe aliotumia wafanyakazi wake kwa njia ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp, Omar Eissa Haroun, mkuu wa halmashauri ya maji katika jimbo hilo la Red Sea, amesema eneo hilo halitambuliki na kwamba mabomba ya umeme na maji yameharibiwa.
Mmoja wa maafisa wa eneo hilo amesema kati ya watu 150 na 200 hawajulikani walipo.
Afisa huyo ameongeza kuwa aliona miili ya wachimba migodi ya dhahabu pamoja na vipande vya vifaa vyao vilivyoharibiwa katika mafuriko hayo na kufananisha maafa hayo na uharibifu uliotokea katika mji wa Derna, mashariki mwa Libya mwezi Septemba mwaka jana wakati maji ya mafuriko yaliposababisha kuporomoka kwa mabwawa, kusomba majengo na kuwauwa maelfu ya watu.
Bwawa la Arbaat ni chanzo kikuu cha maji kwa Port Sudan
Bwawa hilo lilikuwa chanzo kikuu cha maji kwa mji wa Port Sudan, ambao ni makazi ya bandari kuu ya Bahari ya Shamu na uwanja wa ndege unaofanya kazi ambao pia hupokea bidhaa nyingi zaidi za msaada zinazohitajika nchini humo.
Katika taarifa, Chama cha Wanamazingira wa Sudan kimesema mji huo unakabiliwa na tishio la uhaba wa maji katika siku zijazo.
Watu 132 wameuawa kutokana na mafuriko kote nchini Sudan
Hapo jana, jopo kazi la msimu wa mvua nchini humo, lilisema kuwa watu 132 wameuawa kutokana na mafuriko kote nchini humo hii ikiwa idadi iliyoongezeka kutoka watu 68 wiki mbili zilizopita.
Kulingana na mashirika ya Umoja wa Mataifa, mvua za mwaka huu zimesababisha takriban watu 118,000 kupoteza makazi yao.