Taliban waichukuwa Kandahar, mji wa 13 kati ya 34
13 Agosti 2021Ujumbe kupitia Twitter uliotumwa na msemaji wa Taliban siku ya Ijumaa (13 Agosti) ulisema: "Kandahar yote imekombolewa. Wapiganaji wa jihadi wamefikia Uwanja wa Mashujaa."
Madai hayo yalithibitishwa pia na mkaazi mmoja aliyeliambia shirika la habari la AFP kwamba vikosi vyote vya serikali vilikuwa vimekimbilia kwenye kambi moja ya kijeshi iliyo kusini mwa mji huo.
Wabunge wawili, Gul Ahmad Kamin na Arif Noorzai, waliliambia shirika la habari la Ujerumani (dpa) kwamba kabla ya kuweka silaha chini na kukimbia, vikosi vya serikali vilipambana dhidi ya wanamgambo wa Taliban kwa zaidi ya wiki mbili.
Baada ya kufanikiwa kuuchukuwa mji huo wenye wakaazi wapatao 651,000 na ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Afghanistan baada ya mji mkuu, Kabul, sasa wanamgambo wa Taliban waliwa wanadhibiti miji mikuu 13 ya majimbo kati ya majimbo 34 ya Afghanistan.
Taarifa zilisema kuwa sasa serikali ya Rais Ashraf Ghani ilishapoteza sehemu kubwa ya udhibiti, katika kile kinachoonekana kama "ushindi usioelezeka wa Taliban", ambao uliishangaza serikali ya Afghanistan na muungaji wake mkono mkubwa, Marekani.
Marekani, Uingereza zahamisha raia
Taliban walianzisha kampeni yao mara tu baada ya Marekani na washirika wake kuondosha wanajeshi wao nchini Afghanistan, huku Rais Joe Biden akishikilia msimamo wake wa kukomesha miongo miwili ya uvamizi na ukaliaji wa nchi yake kwenye taifa hilo lililovurugwa vibaya kwa vita.
Hayo yakijiri, Marekani na Uingereza ziliamuru kutumwa kwa maelfu ya wanajeshi nchini Afghanistan ili kuwahamisha raia wao.
Amri kutoka Washington na London zilizotolewa usiku wa kuamkia Ijumaa zilitaka mara moja kuondolewa kwa maafisa wa kibalozi na raia kutoka mji mkuu, Kabul.
"Tunapunguza idadi kubwa ya raia wetu mjini Kabul kutokana na hali ya usalama inavyoelekea. Hatua hii haimaanishi kutelekeza. Wala haimaanishi kukimbia. Wala si kujiondowa jumla jamala," alisema msemaji wa Wizara ya Mambo wa Kigeni wa Marekani, Ned Price.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilisema wanajeshi 3,000 wa Marekani wangelitumwa mjini Kabul ndani ya kipindi cha masaa 24 hadi 48, lakini ikisisitiza kwamba wasingelitumika kufanya mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Taliban.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Ben Wallace, alisema nchi yake inatuma wanajeshi 600 kuwaondosha raia wake na wafanyakazi wa zamani wa Kiafghani.
Price alisema pia kuwa Marekani itaanza kutuma ndege kila siku kuwahamisha wakalimani na wafanyakazi wengine wa Kiafghani waliowasaidia Wamarekani.