1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban wakosolewa na EU

14 Agosti 2022

Taliban watimiza mwaka mmoja Jumatatu tangu walipotwaa kwa nguvu madaraka baada ya Marekani na NATO kuondowa wanajeshi Afghanistan

https://p.dw.com/p/4FVx6
Afghanistan | Frauenrechte | Proteste in Afghanistan
Picha: Wakil Kohsar/AFP

Umoja wa Ulaya umelikosoa kundi la Taliban linaloshikilia madaraka nchini Aghanistan.Msemaji wa Umoja huo leo Jumapili amesema kundi hilo limekiuka kwa kiasi kikubwa haki za wanawake na wasichana nchini humo na kuwanyanyasa.

Tamko hilo limetolewa wakati Afghanistan ikielekea mwaka mmoja tangu Taliban kutwaa madaraka. Nabila Nasralli msemaji wa masuala ya mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya amesema Kundi la Taliban limeshindwa kuweka mfumo wa kisiasa unaowajumuisha waafghan wote na hivyo basi kuwanyima waafghanistan kile walichokitaka.

Jumatatu Afghanistan itaadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Taliban walipotwaa madaraka mwaka jana Agosti nchini humo kukishuhudiwa haki za wanawake zikikandamizwa ,uhuru wa vyombo vya habari pamoja na sehemu kubwa ya nchi hiyo ikionekana kutumbukia  katika  umasikini.

Afghanistan | Frauenrechte | Proteste in Afghanistan
Picha: Wakil Kohsar/AFP

Mpaka wakati huu hakuna nchi yoyote iliyoutambuwa utawala wa Taliban na wanawake nchini humo wameingia mitaani kuandamana kulaani vizuizi na sheria zilizowekwa dhidi ya haki yao ya kupata elimu,kufanya kazi na kuwa na uhuru wa kutembea watakako.

Jana Jumamosi yalifanyika maandamano ya amani ya wanawake kadhaa walitembea kwenye mitaa ya mji mkuu Kabul wakisikika kupaaza sauti wakisema  wanataka  chakula,ajira na uhuru,ingawa  kwa mara nyingine yaliingiliwa na  kuzuiwa na  wanajeshi wa Taliban kama ilivyoonekana huko nyuma kwenye maandamano yaliyowahi kufanyika.

Umoja wa Ulaya pia umelaani namna jamii ya Hazaras na shia zinavyofanyiwa nchini humo pamoja na unyanyasaji wa kimifumo wa kuhujumu haki zao katika shughuli zao za kiuchumi,kijamii,kitamaduni ,kiraia na kisiasa.

Afghanistan | Afghanische Frauen kämpfen weiter für ihre Rechte
Picha: Tolo TV

Umoja huo umewahakikishia tena watu wa Afghanistan ahadi yao,ukiutaka utawala wa Taliban kuziondowa sera zinazokiuka haki za binadamu.Umoja huo umesisita kwamba Afghanistan haipaswi kuendelea  kuwa pepo ya magaidi wala kitisho kwa usalama wa kimataifa.

Kundi la Taliban lilitwaa kwa nguvu madaraka mjini Kabul mnamo Agosti 15 mwaka 2021 baada ya Marekani kuchukua uamuzi wa kuondowa wanajeshi wake wakiongoza kikosi cha jumuiya ya kujihami ya NATO ili kumaliza miaka 20 ya ujumbe huo wa NATO kuweko katika taifa hilo.

Vyanzo: DPA/AFP

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW