Taliban yadai kuudhibiti mji katika mpaka na Pakistan
14 Julai 2021Wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan imesisitiza kuwa wamefanikiwa kuzima shambulio hilo na kwamba vikosi vya serikali vimechukua udhibiti, lakini vyanzo vya usalama kutoka upande wa Pakistan vimedai kwamba bendera nyeupe za kundi la wapiganaji wa Taliban zilikuwa zikipepea katika mji huo.
Hali halisi katika mji huo haikuweza kuthibitishwa mara moja lakini picha za kwenye mitandao ya kijamii zimewaonyesha wapiganaji wengi wa Taliban wakiwa wamepumzika katika kile kilichoonekana kuwa eneo la mpaka. Mmoja wa maafisa katika kikosi maalum cha Afghanistan Meja Fazil Mohammad Dawari amesema kuwa
"Maadui hawana uwezo wa kupambana na vikosi maalumu vya Afghanistan. Kama adui anadai kudhibiti eneo, hiyo ni propaganda na wanataka kuhadaa akili za raia. Kwahiyo hakuna tatizo! vikosi maalumu vya Afghanistan na vikosi vingine vimewashinda adui".
Udhibiti wa mpaka wa Spin Boldak ni hatua ya hivi karibuni ya Taliban kuyatwaa maeneo ya mipaka na bandari kavu katika wiki za hivi karibuni. Udhibiti huo unafuatia siku kadhaa za mapiganao makali katika jimbo la Kandahar, ambako serikali ililazimika kusambaza makomando ili kuzuia anguko la mji mkuu wa mkoa hata wakati wapiganaji hao walipokaribia kutwaa eneo linalovuka mpaka.
Msemaji wa wapiganaji Zabihullah Mujahid amewahakikishia wafanyabiashara na wakaazi katika eneo hilo kuwa usalama umeimarishwa huku serikali ikisisitiza kuwa na udhibiti kamili.
Hata hivyo wakaazi wa mji huo wanapinga madai ya serikali, kama anavyosimulia Raz Mohammad kuwa; "nilienda dukani kwangu asubuhi na kuona wapiganaji wa Taliban kila sehemu. walikuwa madukani, makao makuu ya polisi na maeneo ya kawaida. Nimesikia milio ya mapigano maeneo ya karibu".
Mji huo wa mpakani ni moja ya eneo muhimu la kimkakati kwa Taliban. Linaunganisha moja kwa moja jimbo la Balochistan la nchini Pakistan, ambako uongozi wa juu wa wapiganaji umepiga kambi kwa miongo kadhaa, pamoja na idadi isiyojuikana ya wapiganaji wa ziada ambao mara kwa mara huingia Afghanistan ili kusaidia kuimarisha safu zao. Barabara kuu inayotokea mpakani pia inaunganisha mji wa kibiashara wa Pakistan wa Karachi na bandari kubwa katika bahari ya Arabia
Naye rais wa zamani wa Marekani George W. Bush amekosoa uamuzi wa kuviondoa vikosi vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kutoka Afghanistan na kusema raia wameachwa "kuchinjwa" na kundi la Taliban. Bush ameyasema hayo katika mahojiano maalum na DW. Itakumbukwa kuwa rais huyo wa zamani ndiye aliyevituma vikosi vya Marekani nchini Afghanistan mwaka 2001 mara baada ya mashambulizi ya Septemba 11.
Chanzo: AFP