Taliban yadai mashambulizi ya Pakistan yameua 46 Afghanistan
26 Desemba 2024Mashambulizi ya anga ya jeshi la Pakistan yameua watu 46 mashariki mwa Afghanistan, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuongeza hofu ya kuzorota kwa uhusiano kati ya majirani hao wawili.
Hamdullah Fitrat, msemaji msaidizi wa serikali ya Afghanistan, amesema waliouawa katika mashambulizi hayo kwenye maeneo manne ya wilaya ya Barmal, mkoa wa Paktika, walikuwa wakimbizi, na kuongeza kuwa sita walijeruhiwa.
Soma pia: Pakistan yawafukuza wahamiaji wasio na vibali
Mashambulizi hayo yalifuatia taarifa za maafisa wa usalama wa Pakistan kwamba operesheni ya Jumanne ilikuwa ya kuvunja kambi ya mafunzo ya waasi.
Msemaji wa kundi la Tehreek-e-Taliban Pakistan, Mohammad Khurasani, alidai kuwa watu 50, wakiwemo wanawake na watoto 27, waliuawa, na kuwataja kuwa wakimbizi wasio na silaha waliokimbia mashambulizi ya Pakistan.