Tanzania: Chadema na ACT Wazalendo vyakubali kushirikiana
23 Septemba 2020Hata hivyo, wakati vyama hivyo vikitangaza kufikia hatua hiyo, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini humo imeonya kuvichukulia hatua za kisheria vyama vitakavyochukua uamuzi wa kushirikiana bila kufuata matakwa ya sheria.
Huku kampeni za uchaguzi wa rais na ubunge zikiendelea kushika kasi karibu pembe zote za nchi, vyama hivyo vinasema majadiliano yao ya muda mrefu hatimaye yamezaa matunda.
Soma pia: Pigo kwa vyama baada ya wagombea kuenguliwa Zanzibar
Vyama hivyo ambavyo vimewasimamisha wagombea wake wa urais vinachukua hatua hiyo vikilenga kuongeza ushawishi wao kwa wapiga kura hasa wakati huu ambapo kinyang'anyiro hicho cha urais kimewajumuisha wagombea 15.
Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amefichua kuwa hivi karibuni vyama hivyo vitahutubia katika mkutano wa pamoja kubainisha namna ushirikiano huo utakavyoendeshwa.
Je ushirikiano wa Chadema na ACT Wazalendo wakubaliwa?
Ingawa vyama hivyo vinatangaza kuingia kwenye makubaliano hayo wakati tayari kampeni zimepamba moto, wafuatiliaji wengi wa masuala ya uchaguzi wanasema kuwa hatua hiyo ina nafasi kubwa ya kukoleza ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu.
Ezekiel Kamwaga, mwanahabari anayendika mara kwa mara masuala ya uchaguzi na siasa, anasema kuwa vyama hivyo kuamua kuungana mkono katika mbio za urais, kunaweza kukiweka katika wakati mgumu chama tawala.
Wakati vyama hivyo vikiashiria uwezekano wa kuwa na mgombea mmoja, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa imevionya vyama vyovyote vitakavyochukua hatua ya kushirikiana au kuungana bila kufuata sheria, ikisema kwamba vitaadhibiwa.
Katika taarifa yake kwa vyama hivyo, ofisi hiyo ya msajili imevikumbusha kuhusu sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2019, ambayo pamoja na mambo mengine inatamka kuwa vyama vinavyotaka kuungana kwenye uchaguzi vinapaswa kufanya hivyo, miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu na kufikisha makubaliano yao katika ofisi hiyo.
Tanzania yaruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka nchi 15
Hata hivyo, haijafahamika mara moja namna vyama hivyo vitakavyoendesha ushirikiano wao kwenye uchaguzi huu na kwa kiasi gani vitafanikiwa kuvuka kizingiti hicho cha sheria.
Kando na vyama hivyo, chama kingine cha upinzani cha TLP kimetangaza waziwazi kumuunga mkono mgombea urais wa CCM, John Magufuli na kimekuwa kikisambaza mabango yake yanayomuonyesha mgombea huyo na mgombea ubunge wa chama hicho, Augustine Mrema.