1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Tanzania kuendelea na mtazamo wake kuhusu Covid-19

Deo Kaji Makomba8 Machi 2021

Msemaji wa serikali ya Tanzania Hassan Abbas amesema serikali hiyo itaendelea na mtazamo wake wa sasa juu ya kukabiliana na janga la virusi vya corona, na kuwataka wanaoukosoa mtazamo huo kujitazama wao wenyewe.

https://p.dw.com/p/3qMVI
Tansania | Regierungssprecher Hassan Abbas
Picha: Deo Makomba/DW

Msemaji huyo wa serikali amesisitiza niya hiyo ya serikali ya kushikilia msimamo wake, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma ambapo pia aligusia mipango mingine ya serikali.

Msimamo huo, ambao unahusisha kutotoa takwimu zozote kuhusu vipimo vya ugonjwa wa covid-19, umekuwa ukikosolewa ndani na nje ya Tanzania.

Daktari Hassan Abass amesema kuwa wao kama serikali  hawawezi kusema Tanzania haina Corona na kuongeza kuwa serikali hiyo imejitahidi na inaendelea kupambana na ugonjwa huo kwa mbinu mbalimbali.

Soma pia: Serikali ya Tanzania yaonya kuhusu kutoa taarifa za COVID

Amewataka Watanzania wasitiwe hofu bali waendelee kuchukua tahadhari za kiafya kama zinavyoelekezwa huku wakiendelea kuchapa kazi.

Tansania | Regierungssprecher Hassan Abbas
Msemaji wa serikali ya Tanzania Hassan Abbas.Picha: Deo Makomba/DW

Katika siku za hivi karibuni kumeripotiwa vifo vingi vikielezwa kutokana na tatizo la kushindwa kupumua, tatizo ambalo linaelezwa kusababishwa na virusi vyaCorona.

Viongozi wa dini wamejitokeza wakisema wao kama viongozi wanao wajibu wa kulinda uhai wa watu, hivyo hawawezi kukaa kimya kuhusiana na changamoto ya ugonjwa wa Corona unayoikabili dunia nzima ikiwemo nchi ya Tanzania.

Soma pia: Hospitali ya taifa Tanzania yazindua huduma ya kujifukiza

Mzozo wa kuzuwiliwa mahindi kuingi Kenya

Katika hatua nyingine serikali ya Tanzania imesema kuwa hakuna taarifa rasmi ya magari yaliyobeba shehena ya mahindi kuelekea nchini Kenya kuzuiliwa katika mpaka wa Namanga, zaidi ya kuona taarifa hizo kwenye mitandao.

Hata hivyo msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania amekiri kuwapo magari yanayozuiwa kupita katika mpaka wa Namanga, na kuelekezwa katika mipaka mingine ikiwemo Holo Holo, hivyo Tanzania itazungumza na Kenya kutaka kujua kuna tatizo gani.