1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Upinzani wataka COVID kuwekwa wazi

Admin.WagnerD5 Machi 2021

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema kimeitaka serikali nchini humo kuweka wazi kuhusu mwenendo wa janga la voirusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3qGMH
Tansania John Mnyika Generalsekretär Oppositionspartei CHADEMA
Picha: DW/Said Khamis

Chadema pia kimeonya kuwa iwapo suala hilo halitatiliwa maanani basi kitachukua hatua ambazo zitakwenda mbali zaidi. Hata hivyo, serikali nchini humo tayari imeonya juu ya wale wanaotoa na kusambaza taarifa kuhusiana na janga hilo, ikisema ni sawa na kujipalia kaa la moto. 

Chama hicho kimehoji ni kwa nini hadi wakati huu serikali imeendelea kukaa kimya bila kutoa takwimu zozote kuelezea ni Watanzania wangapi wameathiriwa na janga na kuhoji pia ni sababu zipi zilizofanya upimaji wa maambukizi hayo usitishwe ilhali ugonjwa wa Covid 19ni janga la kidunia linalopigiwa kelele ulimwenguni kote.

Kauli ya chama hicho kama inaongeza msukumo hoja nyingine kama hizo zilizowahi kutolewa na makundi mengine ikiwamo chama cha wanasheria cha Tanganyika Law Society, Kanisa katoliki na lile la kilutheri Tanzania yaani KKKT, ambayo yanataka uvaaji wa barakoa kuwa ajenda ya lazima kwa wananchi wote.

Katibu mkuu wa Chadema John Mnyika amewaambia waandishi wa habari leo kuwa, ni muhimu jamii ikaelezwa ukweli kuhusiana na janga hili na ukweli huu unaweza kupatikana kupitia taarifa za mara kwa mara juu ya wale wanaopimwa na kudhibitika kukubwa na maambukizi.

Alisema "Tunaitaka serikali iweze kutekeleza kwa haraka zoezi la upimaji na utoaji wa takwimu kwa umma wa watanzania lakini vilevile kwa mashirika ya kimataifa ambayo serikali inawajibika kutia takwimu ikiwemo shirika la afya duniani, ambalo liko tayari kuzisaidia taasisi za ndani kwa upimaji"

Tansania Zanzibar | Medizin gegen Viren
Tanzania inahimiza matumizi ya tiba asili ya kile inachoita maradhi ya changamoto za kupumuaPicha: Adrian Kriesch/DW

Mara ya mwisho Tanzania kutoa takwimu kuhusiana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid 19 ilikuwa Aprili, 2020 na baada ya hapo serikali ilitangaza kuushinda ugonjwa huo kwa neema ya Muungu kupitia maombi maalumu yaliyofanyika nchini kote. Hata hivyo, kwa hivi sasa kumejitokeza kile kinachoitwa ni maambukizi mapya ya ugonjwa huo, ingawa mamlaka zinasema kwamba vifo vingi vinavyoshuhudiwa wakati huu ni vile vinavyotokana na tatizo la upumuaji.

Soma Zaidi: Hospitali ya taifa Tanzania yazindua huduma ya kujifukiza

Chadema imeitaka serikali kubadili gia katika kushughulikia kadhia hiyo ikipendekeza pia kufunguliwa mlilango kwa taasisi nyingine binafsi kuendesha upimaji wa virusi hivyo.

Chama hicho kimetishia kupiga hodi katika taasisi za kimataifa ikiwamo shirika la afya ulimwenguni na WHO pamoja na Umoja wa Afrika,iwapo serikali haitachukua hatua za haraka kuruhusu upatikanaji wa chanjo pamoja uanzishwaji wa upimaji kuhusiana na maambukizi hayo.

Serikali tayari imetoa msimamo wake ikisema inaamini imefanikiwa kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo na imewaonya wale wote wanaotoa na kusambaza taarifa kuhusiana na ugonjwa huo ikisema kufanya hivyo ni sawa na kujipalia kaa la moto.

George Njogopa