1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaanzisha mkakati wa ruzuku ya mbolea

19 Januari 2023

Serikali ya Tanzania imeanzisha mkakati wa ugawaji ruzuku ya mbolea kwa lengo la kuwakwamua wakulima na kuongeza kasi uzalishaji wa sekta hiyo inayotegemewa na wananchi wengi huku rais akiahidi kuikuza sekta hiyo zaidi

https://p.dw.com/p/4MQFW
Tansania Daressalam | State House | Samia Suluhu Hassan, Präsidentin
Picha: Ericky Boniphace/DW

Rais Samia anayehudhuria mkutano wa jukwaa la uchumi duniani unaendelea Davos, Uswisi ameashiria namna sekta ya kilimo inavyotarajia kukua na hiyo inachagizwa na kile alichosema mipango mikakati inayotekelezwa na serikali yake. Anaamini kuwa ifikapo mwaka 2030, sekta hiyo ya kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa taifa itakuwa kwa asilimia 30, ikilinganishwa na ya sasa ambayo ni asilimia 3.6.

Baadhi ya mambo ambayo Rais Samia ameyaanisha yanayotazamwa kama nguzo katika kuchochea ukuaji huo ni pamoja na  mageuzi yanayoendelea kufanywa ndani ya sekta hiyo ya kilimo kama vile uanzishwaji mpango wa vijana kujikita kwenye kilimo na ongezeko la kiwango cha bajeti katika sekta hiyo. Bajeti hiyo ya kilimo kwa mwaka wa fedha 2022- 2023 imeongezeka mara nne ikilinganishwa na ile iliyopita. Ongezeko hilo limeifanya serikali kuwa na uwanja wa kuanza kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima, ruzuku ambayo itamwezesha mkulima kupata mbolea kwa bei nafuu hasa wakati huu ambako bei yake iko juu kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo vita vya Urusi na Ukraine.

Äthiopien Bio Landwirtschaft Natürlicher Dünger
Mbolea asiliaPicha: Shewangizaw Wogayehu/DW

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema serikali itaendelea kuwa macho kufuatilia bei ya mbolea katika soko la dunia ili kumwondolea mzigo mkulima hasa wakati huu ambao kilimo hicho kinatazamiwa kufanywa kuwa cha kisasa. Hivi sasa serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa kilimo unaojulikana kama ajenda 10/30 ikiwa na maana kwamba kilimo kinakuwa biashara ifikapo 2030. Miradi mikubwa ya uchimbaji mabwawa makubwa ya umwagiliaji pamoja na uanzishwaji wa masoko ya kisasa ni sehemu ya mikakati ya kufikia ajenda hiyo. Kulingana na Waziri Bashe, kazi ya kilimo inatazamiwa kuongezeka kwa wastani wa kuridhisha katika kipndi cha mwaka ujao.

Kuna wasiwasi wa mbolea kutoroshwa kimagendo

Licha ya serikali kusisitiza kuwa ruzuku inayotolewa ni mahsusi kwa ajili ya kuwainua wakulima wa Tanzania, kumekuwa na wasiwasi juu ya mbolea kutoroshwa kimagendo katika mataifa ya nje. Waziri Mkuu Kassaim Majliwa akizungumza hivi karibuni na baadhi ya wakulima hao, alionya juu ya mwenendo huo. Kwa miaka mingi kilimo kimekuwa kikitajwa kama ndiyo uti wa mgongo wa taifa, hata hivyo bado sekta hiyo imeendelea kujikongoja kutokana na uwekezaji mdogo unaofanywa. Huenda safari hii hali hiyo ikashuhudiwa ikibadilika kutokana na hatua zinazobainishwa na serikali