Tanzania yasema Rais Magufuli yuko buheri wa afya
12 Machi 2021Baada ya kuzuka hali ya sintofahamu kuhusu mahali aliko rais wa Tanzania John Maguli, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa amejitokeza wazi na kupuuzulia mbali hofu iliyopo. Amewataka Watanzania waendelee kushikamana, kudumisha amani na wapuuze kauli zinazotolewa alizozitaja kuwa ni za chuki kuhusiana na afya ya Rais Magufuli.
”Tuendelee kufanya ibada na kupata mawaidha yanayohamasisha amani na utulivu. Rais Dkt. Magufuli ni mzima wa afya anaendelea na majukumu yake wakati sisi wasaidizi wake tukizunguka kuwahudumia wananchi. Leo nimezungumza naye na anawasalimia.” Amesema Majaliwa
Lakini kiongozi wa upinzani Tanzania anaeishi Ubelgiji Tundu Lissu, akitaja duru za madaktari na usalama, alisema rais Magufuli alipelekwa Kenya katika hospitali ya Nairobi na kisha akapelekwa India.
Na katika kile kilichoonekana kuwa ni ujumbe uliomlenga Lissu, Majaliwa amewashutumu baadhi ya Watanzania ambao hawapo nchini na wamekuwa wakitoa kauli za chuki kwa sababu hawapendi maendeleo ya nchi akidai wanatamani kuona laifa likiporomoka.
”Tuwapuuze baadhi ya Watanzania ambao wamejawa na chuki tu, wamejawa na husda tu na wanatamani kuwachonganisha na kutaka kushuhudua Taifa hili likiporomoka.” Majaliwa ameongeza kwamba ”kuanzia juzi hata leo asubuhi nimeona Watanzania wenzetu wenye husda tena hawako ndani wako huko wanashawishi vyombo vya Kimataifa viseme Rais wa Tanzania anaumwa kajifungia hizo ni chuki tu, husda tu.”
Mapema Ijumaa, chama kikuu cha upinzani CHADEMA kupitia katibu wake mkuu John Mnyika kilitaka ufafanuzi kuhusu hali ya rais kikisema ni haki ya wananchi kujua hali ya rais wao.
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli ana wasaidizi wake kuanzia ngazi ya taifa hadi kijijini na kwamba anafanyakazi kulingana na mpangokazi wake, hivyo amewataka Watanzania waendelee kuwa na amani huku wakiamini Serikali yao.
Matamshi hayo ya Waziri Mkuu pamoja na kauli za balozi wa Tanzania nchini Namibia, Modestus Kiplimba, ni kauli za karibuni rasmi kutolewa kwa serikali tangu wasiwasi ulipozuka mwanzoni mwa wiki hii
Akizungumza katika mahojiano na shirika la utangazaji la Namibia, balozi Kipilimba amesema anafahamu kuwa rais anaendelea vyema na anachapa kazi.
Lakini Majaliwa na Kipilimba hawajatoa maelezo zaidi na hakuna picha zozote za Rais zilizoonyeshwa. Rais Mgaufuli, mwenye umri wa miaka 61, hajaonekana hadharani tangu Februari 27, kitu ambacho kimezusha hofu sio tu ndani ya nchi bali pia nje ya mipaka.