Tanzania yatangaza kudhibitiwa kwa homa hatari ya Marburg
2 Juni 2023Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu ameutangazia ulimwengu kuhusu kudhibitiwa na kumalizika kwa virusi vya homa ya Marburg ambavyo viliripotiwa mkoani Kagera kaskazini magharibi mwa Tanzania na kusababisha vifo vya watu sita kati ya tisa waliobainika kuwa na maambukizi.
Kufuatia kupatikana kwa mafanikio hayo Waziri Mwalimu ameshukuru jumuiya ya kimataifa hususani Umoja wa Ulaya, Marekani na Umoja wa Afrika kwa kutoa misaada mbalimbali iliyotumika katika mapambano hayo ikiwemo kutoiwekea vikwazo nchi hiyo.
Miongoni mwa watu watatu walionusurika kifo baada ya kuambukizwa Marburg ni Mganga wa kituo cha Maruku Dr. Mahona Ndalu mbaye ametoa ushuhuda wa kilichompata.
Watu watano wafariki Tanzania baada ya mripuko wa homa ya Marburg
Ni wapi ugonjwa huu ulitoka?
Swali hili linamuumiza Waziri wa afya Ummy Mwalimu pamoja na hivyo kulazimika kutoa wito kwa watafiti wa ndani na nje kufanya uchunguzi wa kina.
Shirika la Afya duniani kupitia kwa mwakilishi wake nchini Tanzania Dr. Zabron Yoti wametoa pongezi kwa Tanzania kwa namna serikali ilivyochukua hatua za haraka na kufanikiwa kuzuia maambukizi kutosambaa nchini Tanzania na duniani kwa ujumla.
Pamoja na hayo Umoja wa Afrika na chake cha udhibiti wa magonjwa Africa CDC kupitia kwa kaimu mkurugenzi wake nchini Tanzania Dr. Ahmed Ogwell Ouma pamoja na kupongeza kwa namna nchi za Afrika zinavyoshirikiana, amehimiza nchi za Afrika Mashariki kuwa na mpango wa pamoja wa kushughulikia magonjwa ya milipuko.
Ugonjwa wa Marburg umewahi kuikumba nchi ya Uganda kwa mara saba katika nyakati tofauti na kufanikiwa kuudhibiti hali inayoziamsha taasisi za utafiti kufuatilia kwa kina kuhusu chanzo cha ugonjwa huo.
Mwandishi: Prosper Kwigize- DW Bukoba Kagera