Tanzania yatishia kufuta taasisi za dini
29 Desemba 2017Serikali ya Tanzania imetishia kufuta usajili wa taasisi za kidini zinazochanganya masuala ya dini na siasa, baada ya kiongozi mmoja wa dini kuukosoa utawala wa rais wa nchi hiyo John Magufuli katika mahubiri ya Krismasi.
Viongozi wa upinzani nchini Tanzania wamesema uvumilivu wa moani kinzani umekuwa ukipotea kwa kasi tangu Magufuli alipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015, na kuahidi kulifanyia mageuzi taifa hilo la tatu kiuchumi Afrika Mashariki na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi.
Katiba ya Tanzania inalinda uhuru wa kuabudu, lakini taasisi za kidini hulazimika kusajiliwa katika wizara ya mambo ya ndani ili kupata kibali cha kujiendesha kisheria.
Katibu mkuu wa wizara hiyo, Projest Rwegasira alinukuliwa akisema katika siku za hivi karibuni baadhi ya viongozi ama taasisi za dini wamekuwa wakitumia mahubiri yao kuchambua masuala ya kisiasa, suala ambalo ni kinyume cha sheria.