1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tatizo la maji Zimbabwe laendelea kuwa kubwa

Kabogo Grace Patricia13 Agosti 2009

Wananchi wa Zimbabwe wanatakiwa kulipia maji ambayo hawajatumii

https://p.dw.com/p/J98P
Wananchi wa Zimbabwe wakibeba maji waliyochota kisimani mjini Harare.Picha: AP

Manispaa ya Mji wa Harare imekuwa ikikata maji mjini humo, Waziri anayehusika na masuala ya maji, anaiambia manispaa hiyo kurejesha huduma ya maji. Wateja wa maji kwa shughuli za nyumbani na biashara wamekuwa wakiletewa bili za maji huku maji hakuna, na juu ya yote ugonjwa wa kipindupindu umekuwa ukiukumba mji huo wa Harare, nchini Zimbabwe.

Netsai Mutongi, aliyepokea barua kutoka katika manispaa hiyo ikimtaka alipe dola 230 kwa ajili ya bili ambazo hazijalipwa, amesema hawatalipa fedha hizo na watagoma. Hiyo ni sehemu ya dola milioni 22 ambazo Manispaa ya Mji wa Harare imesema zinawadai wateja wa maji. Lakini Mutongi anasema halipi fedha hizo kwa sababu hajawahi hata kuona maji. Mwanamke huyo mkazi wa Harare anasema fedha wanazotozwa haziendani na kiwango cha maji wanachopata.

Tatizo la maji nchini Zimbabwe linazidi kuwa la hatari. Mji wa Harare peke yake unahitaji lita 1,200 za maji kwa siku kwa matumizi ya nyumbani na viwandani. Mradi wa maji wa Morton Jeffrey una uwezo wa kusambaza lita 614 za maji kwa siku na sasa unasambaza kati ya lita 400 na 500 za maji kwa siku.

Wahandisi wanasema mji wa Harare unapoteza zaidi ya asilimia 40 ya maji yanayosambazwa kutokana na kupasuka kwa mabomba. Albert Nhongomhema, Mhandisi wa maji, anasema kuwa nchi hiyo inapoteza mamia ya lita za maji kwa siku yanayovuja kutokana na kuwa na miundombinu mibovu ya mabomba.

Wakaazi wa nchi hiyo wanasema wamekuwa wakilazimishwa kushirikiana huduma ya maji pamoja na punda na wanyama mwitu kwa kuchota maji kwenye vyanzo vya wazi vya maji, hivyo kutishia usalama wa maisha yao kutokana na kukumbwa na magonjwa ya miripuko. Roslyn Matarutse anasema mtu hawezi kuchimba kisima katika eneo lenye watu wengi, isipokuwa katika maeneo ya shule na kanisa. Makanisa mara nyingi yanatoa huduma ya maji kwa wafuasi wake na wao wanaweza kupata maji kutoka kwa watu waliochimba visima isivyo halali, ambapo ndoo moja ya maji inauzwa dola mbili za Marekani na mara nyingine hata dola tatu.

Watu wamegundua kuwa visima vimechimbwa katika makaazi ya rais, makamu wa rais, mawaziri, makatibu wakuu pamoja na maafisa wa juu wa serikali. Uhaba wa maji nchini Zimbabwe mwaka uliopita ulisababisha kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu, ambapo Shirika la Afya Duniani (WHO), lilitangaza kuwa ni mripuko mbaya wa magonjwa kutokea barani Afrika tangu miaka 15 iliyopita.

Sam Sipepa Nkomo, Waziri wa Maji wa Zimbabwe, amesema anaguswa na suala hilo kwani maji ni uhai na kwa sababu kila kitu kinafanyika kama maji yapo. Akizungumza na shirika la habari la IPS, Waziri Nkomo alisema kama maji safi na salama yanakatwa, itawalazimu wananchi kutafuta vyanzo mbadala vya maji, ambavyo vingi huwa vichafu. Kwa mujibu wa Waziri Nkomo, serikali ya Zimbabwe hivi karibuni ilitumia dola milioni 17 kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya mifumo ya maji safi na maji taka mjini Harare, lakini imekiri kuwa matatizo yaliyopo yako nje ya uwezo wa serikali.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (IPS)

Mhariri:M.Abdul-Rahman