1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tatizo la viwanja vitupu kushughulikiwa Afrika Kusini

17 Machi 2012

Kuvijaza viwanja vya michezo ni suala litakalopewa kipau mbele katika fainali zijazo za kombe la Mataifa ya bara la Afrika. Hayo ni kwa mujibu wa kamati andalizi ya dimba hilo maarufu barani Afrika.

https://p.dw.com/p/14MCs
General view of the Estadio de Bata "Bata Stadium" which will host the opening ceremony for the African Nations Cup, in Bata January 17, 2012. The African Nations Cup is being co-hosted by Equatorial Guinea and Gabon from Jan. 21 to Feb. 12. REUTERS/Amr Abdallah Dalsh (EQUATORIAL GUINEA - Tags: SPORT SOCCER)
Sport Fußball African Nations Cup Bata StadionPicha: REUTERS

Mvuzo Mbebe ambaye ni Afisa Mkuu wa kamati andalizi ya Afrika Kusini amesema katika mkutano wake wa kwanza na waandishi tangu alipochukua wadhifa huo kuwa kuwafnya mashabiki kujaa viwanja ni sababu muhimu ya mafanikio katika dimba hilo litakaloandaliwa mapema mwakani. Mbebe alidokeza kuwa Afrika Kusini itafufua baadhi ya sera zilizotumiwa katika ufanisi wa kombe la dunia mwaka 2010 ikiwemo siku maalum za soka kama Ijumaa ili kuongeza hamasa miongoni mwa mashabiki.

Idadi ndogo ya mashabiki wanaotazama mechi uwanjani katika mechi zisizohusisha timu za nyumbani limekuwa tatizo la muda mrefu kwa soka ya Afrika, huku dimba la mwaka huu kule Gabon na Guinea ya Ikweta likishutumiwa kutokana na idadi ndogo ya mashabiki hata katika mechi za maondowano. Waandalizi walikiri kuwa hawakuwa na uwezo wowote kuwashawishi mashabiki hata baada ya kutoa tiketi za bila malipo.

Brazil na FIFA zaafikiana

Brazil na shirikisho la soka ulimwenguni FIFA wameahidi kufanya kazi pamoja katika kufanikisha fainali za dimba la kombe la dunia 2014, baada ya kufanya mazungumzo kati ya kumaliza mzozo kati yao. Kumekuwa na shutuma kuwa nchi hiyo inajikokota katika kufanya maandalizi ya tamasha hilo maarufu la spoti ulimwenguni.

Maandalizi ya fainali za kombe la dunia 2014 yaendelea nchini Brazil
Maandalizi ya fainali za kombe la dunia 2014 yaendelea nchini BrazilPicha: picture alliance/Agencia Estado

Rais wa FIFA Sepp Blatter alisema baada ya mkutano uliodumu takriban saa mbili na rais wa Brazil Dilma Rousseff kuwa watashirikiana katika kuandaa kinyang'anyanyiro cha kuvutia zaidi cha kombe la dunia.

Mazungumzo hayo yalilenga kumaliza mzozo ulioanzishwa mwezi huu na Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke aliyeishutumu Brazil kwa kufanya maandalizi ya kombe la dunia kwa mwendo wa kinyonga. Rais Rousseff alisema serikali ya Brazil itatimiza ahadi zilizotolewa kwa FIFA na aliyekuwa mtangulizi wake Luiz Inacio Lula da Silva, akiongeza kwua ana matumaini Brazil ina uwezo wa kuandaa tamasha hilo.

Barcelona na Real zatenganishwa

Katika ligi ya mabingwa Ulaya, Barcelona na Real Madrid walitenganishwa katika droo ya mechi za robo fainali na nusu fainali ya UEFA Champions League. Mabingwa hao watetezi Barca kwanza ni lazima wawazabe AC Milan kabla ya kuwa na matumaini ya kukutana na Real katika fainali.

Madrid ilipewa APOEL Nicosia ya nchini Cyprus. Chelsea watacheza na Benfica, nao Marseille wakipambana na Bayern Munich. Mechi za mkondo wa kwanza wa robo fainali zitachezwa tarehe 27 na 28 mwezi huu wa Machi na mkondo wa pili tarehe 3 na 4 Aprili. Katika nusu fainali, Marseille au Bayern itawaalika APOEL Nicosia au Madrid katika mkondo wa kwanza. Benfica au Chelsea itacheza nyumbani dhidi ya AC Milan au Barcelona.

Barcelona na Real zilitenganishwa katika awamu ya robo fainali
Barcelona na Real zilitenganishwa katika awamu ya robo fainaliPicha: AP

Mechi za mkondo wa kwanza zitachezwa tarehe 17 na 18 Aprili na kisha mechi za marudiano tarehe 24 na 25 mwezi Aprili.

Chama cha riadha Kenya chaibadili nia

Chama cha Riadha nchini Kenya kimeamua kutumia mashindano ya riadha ya Prefontaine Classic Diamond kule Eugene, Oregon, Marekani mnamo Juni mosi katika kuwachagua wale watakaoshiriki mashindano ya olimpiki katika mbio za mita 10,000 kwa wanaume, badala ya mbio nne zilizopangwa awali. Mwezi uliopita Mwenyekiti wa Chama cha Riadha nchini Kenya Isaiah Kiplagat alisema wanariadha watano wangeshindana katika kila mbio za mita 10,000 na 5,000 za wanawaume na wanawake kule Eugene, Marekani na kisha washindi watatu wa kwanza wakichaguliwa katika kikosi cha Olimpiki.

Hata hivyo Kiplagat amewaambia wanahabari kuwa timu ya wanawake katika mbio za mita 10,000 na timu zote za mita 5,000 wanaume na wanawake zitachaguliwa katika majaribio ya kitaifa nchini Kenya Juni 23. Umauzi huo umejiri baada ya shinikizo kutoka kwa wanariadha wa zamani akiwemo bingwa wa Olimpiki John Ngugi, Paul Tergat na Moses Tanui.

Bingwa wa mbio za mita 800, Mkenya Pamela Jelimo, amerejea tena kwa kishindo
Bingwa wa mbio za mita 800, Mkenya Pamela Jelimo, amerejea tena kwa kishindoPicha: AP

Kwingineko bingwa wa Olimpiki Usain Bolt ataanza rasmi msimu wake wa riadha katika masshindano ya Kimataifa ya Jamaica mnamo Mei tano. Akizungumza kwenye tovuti yake, Bolt alisema ni heshima kubwa kwake kukimbia mbele ya mashabiki wa nyumbani. Kwamba kila mara kunakuwa na msisimuko uwanjani na hivyo atayatumia mashindano hayo kuwaburudhisha mashabiki. Bolt atatumia mbio hizo kujiandaa kwa mashindano ya Olimpiki jijini London mwezi Agosti

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Mohammed Dahman