TEHRAN : Annan kuitaka Iran kusaidia suluhu Lebanon
2 Septemba 2006Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan leo anatarajiwa kuishinikiza serikali ya Iran kusaidia kuimarisha makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hizbollah lakini wanadiplomasia wanasema mazungumzo pia yatahusu mzozo wa nuklea kati ya Iran na mataifa ya magharibi.
Ziara yake hiyo inakuja wakati Marekani ikiongoza harakati za kutaka Iran iwekewe vikwazo baada ya kushindwa kusitisha shughuli zake nyeti za nuklea hapo tarehe 31 mwezi wa Augusti kama ilivyoamuriwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ahmad Fawzi msemaji wa Annan ambaye amekuwemo katika safari ya wiki nzima Mashariki ya Kati pamoja na Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuimarisha makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Lebanon ameliambia shirika la habari la Uingereza reuters kwa njia ya simu kutoka mji mkuu wa Qatar Doha kwamba lengo kuu la ziara hiyo ya Iran ni kuijadili Lebanon.
Hata hivyo amesema suala la mpango wa nuklea wa Iran litazungumzwa kwa uhakika.
Annan anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Waziri wa mambo ya nje wa Iran Manouchehr Mottaki,Rais Mahmoud Ahmedinejad na msuluhishi mkuu wa masuala ya nuklea wa Iran Ali Larijani.