Tehran: Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anafanya mazungumzo Iran
3 Septemba 2006Katika mazungumzo ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, huko Tehran, viongozi wa Iran wameushikilia msimamo wao ule ule kuhusu suala linalobishiwa la nchi hiyo kusafisha madini yake ya Uranium kwa ajili ya kujipatia nishati ya kinyukliya. Hayo yameelezwa wazi pale Kofi Annan alipokutana jana na waziri wa mambo ya kigeni, Manucher Mottaki, mshauri mkuu wa masuala ya atomiki, Ali Larijani, na rais wa zamani wa Iran, Akbar Hashemi Rafsanjani.
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi za Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuipa Iran wiki mbili zaidi ifafanuwe msimamo wake.
Lakini Bwana Mottaki aliahidi kwamba nchi yake itatoa ushirikiano katika kuwekwa majeshi ya Umoja wa Mataifa kusini mwa Libanon. Ili kuhakikisha amri ya kusitisha mapigano inafanya kazi huko Libanon, siku za mbele Iran haitawapatia silaha zaidi wanamgambo wa Hizbullah.
Bwana Kofi Annan aliyaelezea mazungumzo yake huko Iran kuwa yalikuwa mazuri na yenye manufaa. Leo katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amepangiwa akutane na Rais Mahmud Ahmadinejad.