Tel Aviv. Israel na Palestina wawakumbuka viongozi wao.
13 Novemba 2005Nchini Israel , kiasi cha watu 200,000 wamehudhuria maandamano ya kumbukumbu katika eneo la wazi la mjini Tel Aviv ambako waziri mkuu wa zamani Yitzhak Rabin aliuwawa miaka kumi iliyopita.
Rabin alipigwa risasi na kufa na kijana mmoja wa Kiyahudi mwenye imani kali ambaye alikuwa akipinga juhudi za waziri mkuu huyo za kuleta amani na Wapalestina.
Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton amesifu ushupavu wa Rabin na kazi aliyofanya kwa ajili ya manufaa ya Wapalestina na Waisrael.
Rabin , pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa wakati huo Shimon Peres pamoja na kiongozi wa Wapalestina marehemu Yasser Arafat walikuwa kwa pamoja washindi wa tuzo ya amani ya Nobel kutokana na juhudi zao za zilizosababisha kufikiwa kwa makubaliano ya amani ya Oslo.
Kumbukumbu hiyo imeingiliana na sherehe kama hizo mjini Gaza ambapo Wapalestina wanafanya kumbukumbu ya mwaka wa kwanza tangu kufariki kwa kiongozi wao Yasser Arafat. Alifariki Novemba 11, 2004 katika hospitali nchini Ufaransa.