Tel Aviv. Waziri mkuu wa Israel kukutana na rais wa Palestina mwezi huu.
4 Juni 2005Ofisi ya waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon imesema kuwa Bwana Sharon atakutana na rais wa Palestina Mahmoud Abbas mjini Jerusalem baadaye mwezi huu. Utakuwa mkutano wao wa kwanza kati ya kiongozi wa Israel na Palestina katika mji huo ambao uko katikati ya mzozo wa mashariki ya kati.
Mmoja kati ya watu mashuhuri wanaoendesha majadiliano ya amani kutoka upande wa Wapalestina Saeb Erekat, hakuweza kuthibitisha mahali pa mkutano huo lakini amesema kuwa mkutano huo utafanyika katika eneo hilo.
Ofisi ya Bwana Sharon pia imesema waziri mkuu huyo amemtakia Bwana Abbas kupona kwa haraka, baada ya kufanyiwa upasuaji katika kusafisha mshipa wa damu siku ya Jumatano.
Bwana Abbas amepelekwa hospitali katika mji mkuu wa Jordan Amman , baada ya kupata hali ya uchovu na maumivu kifuani.