The Daily Monitor lipo huru kuchapishwa Uganda
30 Mei 2013Redio mbili zinazomilikiwa na gazeti hilo K-FM na Dembe FM nazo pia zimefunguliwa. Hata hivyo Gazeti jengine la Red Pepper ambalo pia lilifungwa bado halijafunguliwa lakini waziri Onek anasema mazunguumzo kati ya gazeti hio na serikali yanaendelea.
Akizungumza na waandishi habari mjini Kampala alisisitiza kuwa gazeti la The daily monitor lilivunja sheria ya usiri na kwa kufanya hivyo walikuwa wanahatarisha usalama wa nchi. Hio ndio sababu polisi ikaamua kutumia nguvu kuitafuta barua iliyoandikwa na mkuu wa vitengo vya ujasusi akidai kuwa kulikuwa na njama ya kuwauwa baadhi ya maafisa wakuu wa serikali na jeshi wanaopinga mpango wa Rais Yoweri Museveni wa kumwachia mamlaka mwanawe Brigedia Muhoozi Kaneirugaba.
Polisi wamendoka katika ofisi za gazeti
Baada ya siku kumi za vuta ni kuvute kati ya serikali na wakuu wa gazeti la The daily monitor, waziri Hillary Onek akatangaza kuwa polisi imewaondoa askari wake kwenye ofisi za The daily monitor ili waendelee na kazi zao kama kawaida wakati polisi ikiendelea na upelelezi wao na upekuzi.
Waziri Onek anasema wamelifungua gazeti hili baada ya wakuu wa gazeti hili kuomba msamaha kwa kuchapisha barua ambayo serikali inasema inahatarisha usalama wa nchi.
"Walituahidi kuwa gazeti la Monitor litachapisha ripoti ambazo wamezipata kwa njia inayofaa na za haki, pia watahakikisha ripoti zote watakazochapisha hazitaegemea upande wowote, hazitaibua hali ya wasi wasi nchini au kuchochea ukabila na chuki. Walituahidi kuwa hawatachapisha ripoti ambazo zitahatarisha usalama wa nchi na kutilia mkazo kuwa watakuwa wanazikagua kwa makini ripoti zinazohusu usalama wa nchi kabla ya kuchapishwa". alisema waziri Hillary Onek.
RedPepper bado kizuizini
Kuhusu kuendelea kufungwa gazeti la RedPepper, waziri Onek ameelza "Tumekuwa tukizungumza na RedPepper na leo tutakutana nao tena ili tuone ni vipi tunaweza kushirikiana. Ikiwa tutakubaliana nao kuwa watakuwa wanafanya kazi kulingana na sheria, hatutakuwa na shida kuwaruhusu waendelee kuchapisha".
Tukienda hewani, shirika la kutetea haki za waandishi habari nchini Uganda lilikuwa mahakamani kumshtaki mkuu wa polisi, mkuu wa sheria pamoja na taasisi ya mawasiliano kwa kukandamiza haki ya waandishi habari ya kuwa huru wanapofanya kazi yao. Sikiliza ripoti ya Leylah Ndinda kwa kubonyeza alama ya kusikiza masikioni hapo chini.
Mwandishi: Leylah Ndinda
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman