1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuandaa mipango ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya

20 Julai 2016

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May anaanza ziara katika mataifa ya Ujerumani na Ufaransa ikiwa ni sehemu ya kuanza mipango ya taifa hilo kujiondoa rasimi katika Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1JSUK
Waziri Mkuu wa Uingereza,Theresa May
Waziri Mkuu wa Uingereza,Theresa MayPicha: picture-alliance/abaca

Katika ziara yake hiyo ya kwanza ya nje ya nchi tangu achukue madararaka ya uwaziri mkuu Theresa May anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Berlin na hapo kesho (21.07.2016) atazuru Ufaransa ambapo atakuwa na mazungumzo na Rais wa Ufaransa Francois Hollande. Mazungumzo hayo yana lengo la kuandaa mazingira ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May anatarajiwa kujenga mahusiano na viongozi hao na pia kuwaeleza juu ya umuhimu wa serikali yake kuhitaji muda kushauriana zaidi kabla ya kuanza kuchukua hatua za kujiondoa rasmi katika Umoja wa Ulaya.

" Ni matarajio yangu kuwa Uingereza itafanikiwa katika hatua yake ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ndiyo maana nimeamua kuanza na ziara ya kutembelea Ujerumani na Ufaransa mapema tu baada ya kushika madaraka" alisema Theresa May katika taarifa yake.

Akiri juu ya changamoto zilizopo

Kiongozi huyo aliongeza kuwa hapuuzi changamoto wanazokabiliana nazo katika majadiliano ya mchakato wa kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya na kusema hatua ya kuweza kuweka bayana masuala wanayokabiliana nayo ni sehemu muhimu katika mazungumzo hayo.

" Nataka kutoa ujumbe juu ya umuhimu wa mahusiano na washirika wetu ndani ya Umoja wa Ulaya na siyo tu katika kipindi hiki bali hata wakati ambapo tutakuwa tayari tumejiondoa kwenye Umoja wa Ulaya" alisema May.

Moja ya masuala muhimu yatakayochukua nafasi katika mazungumzo hayo yanayohuasiana na mchakato wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya ni pamoja na uhuru wa kusafiri na muda wakuanza utekelezaji wa ibara ya 50 kuhusiana na mkataba wa Lisbon juu ya kuanza rasmi kipindi cha miaka miwili cha mchakato wa Uingereza kujitoa kwenye Umoja huo.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/M. Gambarini

"Waziri Mkuu Theresa May anatarajiwa kujenga mahusiano na viongozi wenzake wa ulaya, kufahamiana nao kwa ufasaha zaidi na pia kuelezea msimamo wa Uingereza kuhusiana na suala la Brexit huku akitumia umahiri wake katika kuhimiri majadiliano hasa katika kufanikisha jambo analotaka" alisema Professor Iain Begg mmoja wa wachambuzi ambaye ni mhadhiri wa masuala ya uchumi katika chuo kikuu cha masuala ya Uchumi cha mjini London "

Wakati baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya yakitaka Uingereza ijiondoe haraka kwenye Umoja huo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametaka ipewe muda ili iweze kujiandaa vema kabla ya kuanzisha utaratibu wa kujiondoa rasmi.

Hata hivyo Kansela Merkel ameonya kuwa Uingereza haiwezi kuendelea kufaidi soko la pamoja ndani ya Umoja wa Ulaya wakati ikipingana na suala la uhuru wa kusafiri kwa wakazi wa Umoja huo wanaotaka kwenda Uingereza kwa utaratibu wa mfumo huru wa kusafiri ndani ya Umoja wa Ulaya.

Mwandishi : Isaac Gamba/ AFPE/ DPAE

Mhariri : Gakuba Daniel