Theresa May aitisha uchaguzi wa mapema
18 Aprili 2017Akisimama nje ya ofisi yake katika mtaa wa Downing, May alisema alisita juu ya kuliomba bunge kuunga mkono hatua yake hiyo kuitisha uchaguzi na mapema, kutoka mipango ya awali ya kuitisha uchaguzi huo mwaka 2020, lakini aliamua ni muhimu kupata uungwaji mkono kwa juhudi za chama chake tawala cha Conservative kuendelea na hatua za Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya. Baadhi wameshangazwa na hatua yake, amekuwa akisema mara kwa mara hataki kuvurugwa na kampeni itakayopoteza muda, lakini uchunguzi wa maoni ya wapiga kura unamuonesha akiwa anaongoza, uchumi unakwenda vizuri licha ya kura ya Brexit na amekabiliana na upinzani kutoka katika chama chake binafsi kutokana na mageuzi ya ndani.
Sarafu ya pauni imepanda kwa kiwango cha juu cha miezi miwili na nusu dhidi ya dola ya Marekani baada ya kutangaza uchaguzi, lakini faharasa kuu ya soko la hisa nchini Uingereza iliporomoka katika kiwango chake cha chini kabisa katika muda wa zaidi ya wiki saba. Uingereza inajiunga na orodha ya nchi kadhaa za Ulaya zinazopanga kufanya uchaguzi mwaka huu. Uchaguzi nchini Ufaransa mwezi Aprili na Mei na Ujerumani mwezi Septemba una uwezekano wa kuelekeza taswira ya kisiasa katika miaka miwili ijayo ya majadiliano ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya wakati mazungumzo yanatarajiwa kuanza rasmi katika mwezi wa Juni.
Wapinzani wa Labour mashakani
Wajumbe wa majadiliano wa Umoja wa Ulaya wanamatumaini kwa hatua hiyo ya waziri mkuu wa Uingereza itampa nguvu zinazostahili akiwa na mamlaka ya wazi kuweza kutoa masharti ya uingereza kujitoa kutoka Umoja huo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema ana matumaini uchaguzi wa mapema utaelekeza katika uwazi na uwajibikaji katika majadiliano ya Uingereza pamoja na umoja wa Ulaya kuhusiana na Brexit.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uingereza cha Labour, Jeremy Corbyn amesema anaupokea uamuzi wa waziri mkuu May. "Naikaribisha fursa hii, kwetu sisi kuweza kuwaeleza Waingereza kusimama dhidi ya serikali hii na ajenda yake iliyoshindwa ya kiuchumi, ambayo imesababisha matatizo katika huduma za afya, mashule kupata fedha chache, pamoja na kuwaacha watu wengi hawana hakika. Tunataka kuwaelezea wananchi wa Uingereza, kuhusu jamii inayomjali kila mtu, uchumi unaofanyakazi kwa kila mtu, na Brexit inayofanyakazi kwa kila mtu."
Nae waziri kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon amesema hatua ya waziri mkuu May inaakisi dhamira yake kuipeleka Uingereza katika mrengo wa kulia wa kisiasa wakati nchi hiyo ikijadili kuhusu Brexit kutoka Umoja wa Ulaya. Sturgeon amesema May anachukua fursa ya mtafaruku mkubwa katika chama cha Labour ili kuzima upinzani na kuwatenga watu ambao wanampinga. "Hatua hii itakuwa na maana sio tu uwezekano mgumu wa Brexit, lakini kubana zaidi matumizi na upunguzaji mkubwa wa bajeti. Kwa hiyo katika Scotland ni muda sasa wa kuhakikisha kwamba tunasimama kwa ajili ya maslahi ya Scotland, kuifanya sauti ya Scotland kusikka na kuhakikisha wabunge wanapigania maslahi ya Scotland."
Utaratibu wa serikali nchini Uingereza kuitisha uchaguzi mpya una utata mkubwa kuliko ilivyozoeleka hapo kabla. Serikali zilikuwa na uwezo wa kuitisha uchaguzi kama zitakavyo, lakini sheria ya bunge ya muda maalum, iliyopitishwa mwaka 2021 , imeweka vipindi maalum kufanyika uchaguzi kila baada ya miaka mitano. Chini ya sheria hiyo, hoja ya uchaguzi mpya kabla ya wakati inapaswa kupelekwa bungeni na kukubaliwa na theluthi mbili ya wabunge 650 katika baraza la wawakilishi, ikiwa ni pamoja na viti ambavyo havina wabunge. May amesema atawasilisha hoja hiyo bungeni kesho Jumatano. Iwapo itapita, bunge litasitisha shughuli zake siku 25 kabla ya siku ya Uchaguzi.
Mwandishi: Sekione Kitojo/rtre
Mhariri: Grace Kabogo