1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May ajiandaa kuwa waziri mkuu

13 Julai 2016

Theresa May hii leo atakuwa waziri mkuu wa pili mwanamke katika historia ya Uingereza, wakati David Cameron akiondoka madarakani baada ya wapiga kura wa Uingereza kuamua kujitoa katika Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/1JO5S
Großbritannien London Theresa May
Picha: Getty Images/J. Taylor

Waziri Mkuu David Cameron atahudhuria kikao cha mwisho cha kujibu masuali bungeni kabla ya kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth wa pili katika Kasri la Buckingham.

Malkia kisha atamtaka May, ambaye kwa sasa ni waziri wa mambo ya ndani, kuunda serikali na waziri huyo mkuu mteule atatoa taarifa nje ya makaazi yake mapya ya Downing Street. Viongozi wa Ulaya wameitaka serikali ya Uingereza kuharakisha mchakato wa kujitoa rasmi katika umoja huo, lakini May amedokeza kuwa hatauharakisha mpango huo, mashuhuri kwa jina la Brexit.

May, aliye na umri wa miaka 59, atakuwa waziri mkuu wa pili mwanamke wa Uingereza baada ya Margaret Thatcher ambaye kila mara hulinganishwa naye. Lazima ajaribu kutuliza migawanyiko iliyopo ndani ya Chama cha Kihafidhina na kukabiliana na uwezekano wa mtikisiko wa kiuchumi.

Changamoto nyingine kubwa ni pamoja na kuizuia Scotland inayounga mkono Umoja wa Ulaya dhidi ya kuitisha kura ya uhuru wake ili kubakia katika Umoja wa Ulaya, na kuimarisha mahusiano mapya ya kibiashara na kidiplomasia ili kujiandaa kwa hali ya baadaye ya baada ya Brexit.

Großbritannien Innenministerin Theresa May & Premierminister David Cameron
May anamrithi Cameron katika wadhifa wa waziri mkuuPicha: picture-alliance/empics/N. Ansell

Waziri wa Afya wa Uingereza, Jeremy Hunt, amesema anaamini Uingereza sasa imepata Angela Merkel wao: "Nadhani tunaweza kuhakikisha kuwa nchi hii inapendeza zaidi, inasisimua, na yenye uchumi wa kijasiriamali katika ulaya nzima. Itachukua miaka kadhaa kutimiza hilo lakini tuna changamoto kubwa katika miaka michache ijayo wakati tukitafuta mikataba mipya ya biashara, na nadhani katika baraza la mawaziri jana hisia zilikuwa ni tumempata Angela Merkel wetu.

Kura ya Brexit ilifichua kiwango kikubwa cha kukosekana kwa usawa katika jamii ya Uingereza, ambayo May ameahidi kushughulikia na kuugeuza ulingo wa siasa, kwa kutumbukiza chama chake cha Kihafidhina na chama kikuu cha upinzani cha Labour katika mtikisiko.

Kiongozi anayekabiliwa na shinikizo Jeremy Corbyn, ambaye aliyeshutumiwa kwa kushindwa kuwashawishi wapiga kura wa tabaka la wafanyakazi kuunga mkono uwanachama wa Umoja wa Ulaya, sasa anakabiliwa na kinyang'anyiro kikali cha uongozi. Hapo jana, Owen Smith alikuwa mgombea wa pili baada ya mbunge mwenzake Angela Eagle kujiunga katika katika kinyang'anyiro cha kujaribu kumwangusha msoshalisti huyo mkongwe.

May wakati huo huo, anatarajiwa kuanza kutangaza baraza lake la mawaziri baadayae leo, akiwemo waziri wa Brexit atakayeshughulikia mazungumzo ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Wanawake wanatarajiwa kuzoa nyadhifa kadhaa kubwa, kwa mujibu wa vyombo vya habari, miongoni mwao ni waziri wa sasa wa nishati, Amber Rudd. Hata hivyo, waziri wa mambo ya kigeni Philip Hammond, kiongozi aliyefanya kampeni za Brexit, Chris Grayling, ambaye ni kiongozi wa Wahafidhina Bungeni na Justin Greening, wa wizara ya maendeleo ya kimataifa wanatazamiwa kubakia na nafasi zao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef