Theresa May akabiliwa na upinzani katika mpango wa Brexit
12 Oktoba 2018Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May imesisitiza kuwa haitaiweka Uingereza mtegoni katika suala la umoja wa forodha usio na kikomo na Umoja wa Ulaya baada ya kujitenga, mwezi M4echi mwaka ujao. Hata hivyo msemaji wake amekataa kuthibitisha kwamba mpango wa kuuachia wazi mpaka wa ardhi na Ireland baada ya Uingereza kujiondoa mwezi Machi mwaka 2019 utakuwa wa muda mfupi.
Majadiliano mjini Brussels yamepiga hatua kabla ya kufanyika mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya wiki ijayo, na May aliwaeleza baadhi ya wanachama katika baraza lake la mawaziri Alhamisi kuhusu jinsi anavyopanga kupata makubaliano. Uingereza imependekeza utaratibu wa forodha na Umoja wa Ulaya ili kuzuia ukaguzi wa kimwili kati ya Ireland Kaskazini na Ireland mwanachama wa Umoja wa Ulaya , hadi suala hilo litakaposuluhishwa na makubaliano ya biashara pana.
Mbunge mmoja mkosoaji katika chama cha Conservatives chake Theresa May, Andrea Jenkyns amekiomba chama hicho kumteua kiongozi mpya iwapo May ataendelea na mpango huo wake wa Brexit, na kuutaja kuwa usaliti mkubwa wa kura ya Uingereza kutaka kujitenga na Muungano wa Ulaya. Wito wa Jenkins unafuatia upinzani wa baadhi ya mawaziri wakuu jana Alhamisi wakati May alipowaeleza mawaziri wake kwamba makubaliano ya kihistoria ya Brexit yanakaribia.
May anataka makubaliano ya biashara ya siku zijazo kuwa tayari ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka 2021. Chama cha Democratic Unionist kimetishia kuiangusha serikali iwapo mpango wa may utasabanisha kuwepo kwa vikwazo vya biashara kati ya Ireland Kaskazini na Uingereza bara.
Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Ulaya Jean Claude Junker amesema inawezekana makubaliano ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya yakapatikana kati mkutano wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wiki ijayo mjini Brussels, na mwengine mwezi Novemba, lakini suala la Ireland linabakia kuwa la kutatanisha.
Mwandishi: Sophia Chinyezi
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman