Theresa May kumrithi David Cameron Uingereza
12 Julai 2016Hii ni baada ya mpinzani wake Andrea Leadson kusitisha kwa ghafla kampeni yake ya wadhifa huo.
May mwenye umri wa miaka 59, atamrithi David Cameron, aliyetangaza kuwa anajiuzulu baada ya Waingereza mwezi uliopita kupiga kura ambayo haikutarajiwa ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Mpango wa Uingereza kujitoa umeidhoofisha umoja huo wa nchi wanachama 28, kusababisha hali ya sintofahamu kuhusiana na biashara na uwekezaji na kuyumbisha masoko ya fedha.
Theresa May na Andrea Leadsom walitarajiwa kupambana katika uchaguzi wa mashinani wa wanachama wa chama cha Kihafidhina, huku matokeo yakitangazwa Septemba 9.
Lakini Leadsom alijiondoa ghafla jana baada ya kampeni yake kugubikwa na matamshi yaliyozusha utata kuhusu mpinzani wake kutokuwa na watoto na maswali kuhusu kama alidanganya katika wasifu wake. Akizungumza baada ya kuthibitishwa kuwa Waziri Mkuu mtarajiwa, May alisema "Tunahitaji kuiunganisha nchi yetu na tunahitaji maono mapya, yaliyo bora na imara kwa mustakabali wa nchi yetu. Maono ya nchi yetu yanayofanya kazi sio tu kwa wachache wanaojiweza, lakini pia kwa kila mmoja wetu, kwa sababu tutawapa watu udhibiti zaidi wa maisha yao, na kuijenga Uingereza bora".
Cameron aliwaambia wanahabari kuwa ataongoza kikao chake cha mwisho cha baraza la mawaziri leo na kujibu maswali bungeni kesho Jumatano kabla ya kuikabidhi barua ya kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth. May atakuwa waziri mkuu wa pili mwanamke nchini Uingereza baada ya Margaret Thatcher.
Ushindi wake una maana kuwa mchakato mgumu wa kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya utaongozwa na mtu kutoka upande wa kampeni iliyoshindwa. Anasema Uingereza inahitaji muda wa kuutafakari mkakati wake wa kujiondoa na haipaswi kuwasilisha rasmi mpango huo kabla ya mwisho mwa mwaka huu.
May alisema katika hotuba yake jana kuwa hapatakuwa na kura ya pili ya maoni na hakuna jaribio la kujiunga tena katika Umoja wa Ulaya kupitia mlango wa nyuma. "Ipo haja ya uingozi thabiti, unaoweza kutuondoa katika wakati mgumu na usiotabirika wa hali ya kiuchumi na kisiasa. Haja ya kusimamia mpango bora wa Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya, na kujiwekea nafasi mpya katika ulimwengu. Brexit ina maana Brexit na tutaitumia kupata mafanikio".
Ikulu ya White House imesema Rais wa Marekani Barack Obama ana matumaini kuwa “mahusiano maalum” baina ya Marekani na Uingereza yataendelea baada ya May kuapishwa kuwa waziri mkuu.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema viongozi wa ulaya watakuwa na mazungumzo magumu na Uingereza akisisitiza kuwa nchi hiyo haitaweza kuingia kwa njia huru katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya bila kukubali uhamiaji huria wa watu.
Naye kamishena wa Uchumi katika Umoja wa Ulaya Pierre Moscovici amesema mazungumzo yanapaswa kuanzishwa haraka iwezekanavyo ili kupunguza hali iliyopo ya sintofahamu.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri:Josephat Charo