1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Thomas Tuchel abeba lawama kufuatia kipigo cha 3-0

12 Februari 2024

Thomas Tuchel amesema wachezaji wake walifanya maamuzi mabaya na kukata tamaa katika pambano dhidi ya Bayer Leverkusen uwanjani Bay Arena. Hata hivyo anaamini kuwa bado wana uwezo wa kuchukua tena ubingwa msimu huu.

https://p.dw.com/p/4cK0F
Kocha wa Bayern Munich Thomas Tuchel
Kocha wa Bayern Munich Thomas TuchelPicha: Peter Schatz/picture alliance

Bayer Leverkusen imefungua mwanya wa alama tano kati yao na Bayern Munich baada ya kutembeza kichapo cha 3-0 mbele ya mabingwa hao watetezi, ugani Bay Arena siku ya Jumamosi.

Kocha Xabi Alonso ameeleza furaha juu ya maendeleo mazuri ya timu yake msimu huu. Alonso hata hivyo ametahadharisha wachezaji wake kutolegeza kamba katika mechi 13 zilizosalia.

Alipoulizwa kuhusu nafasi ya Bayer Leverkusen kuchukua ubingwa, Xabi Alonso amesema, "Ushindi huu unamaanisha kuwa, kuna tofauti ya alama tano tu kwa sasa. Nafikiri tumesalia na mechi 13 au 14 hivi, haimaanishi chochote. Hatufikirii kuhusu ubingwa."

Soma pia: Ulimwengu wa soka waomboleza kifo cha nguli wa soka wa Ujerumani Beckenbauer

Kiungo mzoefu wa Bayern Munich Thomas Mueller amewakosoa wachezaji wake kwa kukosa ujasiri katika mchezo huo.

Mueller mwenye umri wa miaka 34, amemtetea kocha wake Thomas Tuchel akisema kamwe hapaswi kulaumiwa.

"Bado kuna mechi nyingi, tuna malengo yetu. Kupoteza mchezo wa leo ni pigo kubwa kwetu bila shaka. Tulitaka kuwa na matokeo tofauti lakini lazima tukubali kilichotokea, tutasimama na kujipanga upya," ameeleza Thomas Tuchel.

Kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka minane, Bayern Munich ambao ni mabingwa mara 11 mfululizo wa Bundesliga, walifanikiwa kupiga shuti moja tu lililolenga lango.