1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tikiti za mwisho za Kombe la Afrika

17 Novemba 2014

Nigeria, Cote d'Ivoire na Ghana zinakodolewa macho na michuano muhimu ya mwisho ya kufuzu katika Kombe la Mataifa ya Afrika, na labda kuepuka fedheha ya kubakia nje ya mashindano hayo

https://p.dw.com/p/1Dojo
Bildergalerie Afrikanische Fußballspieler Stephane Mbia
Picha: Getty Images/C. Brunskill

Nchi hizo tatu ni miongoni mwa sita za mwisho zitakazojiunga na nyingine kumi katika mashindano hayo. Tikiti hizo zitaamuliwa katika michuano ya mwisho Jumatano wiki hii, wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Congo Brazaville, Uganda na Malawi pia zikiwa na nafasi ya kufuzu. Nigeria itaweza kufuzu kama itaizaba Afrika Kusini ambayo tayari imefuzu. Matokeo mengine yoyote yataipa nafasi Jamhuri ya Congo kufuzu.

Cote d'Ivoire itapambana na Cameroon wakihitaji sare tu ili kufuzu mbele ya Congo. Malawi inaweza kufuzu kama matokeo yake dhidi ya Ethiopia yatakuwa bora zaidi kuliko ya Mali itakayochuana na Algeria. Algeria, Cape Verde, Tunisia, Afrika Kusini, Zambia, Cameroon, Burkina Faso, Gabon na Senegal tayari zimefuzu pamoja na wenyeji Guinea ya Ikweta

Viongozi wa Shirikisho la Kandanda Afrika – CAF walishusha pumzi baada ya Guinea ya Ikweta kukubali ombi lao la kuitaka iwe mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika hapo mwakani, lakini hatua hiyo imezusha mchanganyiko wa hisia miongoni mwa raia wa taifa hilo dogo la Afrika Magharibi.

Kuwasili ambako hakukutarajiwa kwa tamasha la Kombe la Mataifa ya Afrika katika kipindi cha chini ya miezi miwili nchini Guinea ya Ikweta yenye utajiri wa mafuta kumezusha hofu kuhusiana na ugonjwa wa Ebola. Taifa hilo dogo lilikubali katika muda wa mwisho mwisho kujitwika mzigo wa kuandaa mashindano hayo mwaka wa 2015 baada ya Morocco kupokonywa kibali baada ya kusisitiza kuwa hauwezi kuandaa kutokana na Ebola.

Europa League Mönchengladbach vs Limassol 23.20.2014
Nahodha wa timu ya taifa ya Guinea Ibrahima Traore anachezea timu ya Borussia MoenchengladbachPicha: Reuters/Wolfgang Rattay

Alfredo Okenvo ambaye ni kiongozi wa mashirika ya raia katika mkuu wa pili nchini humo wa Bata anasema kukubali wito wa kuwa mwenyeji wa dimba hilo kunazisha wasiwasi mkubwa. Anasema haiingii akilini kuwa serikali ilikubali kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, hasa ikizingatiwa muda mfupi ilionao kufanya hivyo. Anasema wasiwasi wake siyo tu ugonjwa wa Ebola, lakini pia uwezo wa nchi hiyo kuwa tayari kuandaa michezo hiyo kuanzia Januari 17.

Naye Brigida Bidang ambaye ni muuguuzi hakubaliani na hatua ya nchi yake kuchukua jukumu hilo, kwa sababu Kombe la Mataifa ya Afrika huwavutia mashabiki wengi hivo kitisho cha Ebola kitakuwa kikubwa mno.

Agnes Esidang, mmiliki wabaa katika mji mkuu Malabo, anameza mate akisubiri kwa hamu kuwasili wageni kwa ajili ya biashara yake. Anasema kuandaliwa kinyang'anyiro hicho nchini mwao ni habari njema sana.

Uamuzi uliochukuliwa na rais Teodoro Obiang na kushutumiwa na baadhi ya makundi ya haki za binaadamu, hata hivyo ulipata uungwaji mkono na rais wa kundi la kiraia la Rebirth Africa, Souleymane Anta Ndiaye. Ndiaye anasema hatua hiyo inaonyesha nia ya ushirikiano mzuri barani Afrika.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Rueters
Mhariri: Yusuf Saumu