Tillerson na Lavrov, watakutana Afrika kweli?
8 Machi 2018Lakini hakuna dalili kwamba hilo litafanyika licha ya kuwa viongozi hao walifikia katika hoteli moja mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Wanadiplomasia hao wakuu wa Marekani na Urusi wanaonekana kuzungukana tu huko Afrika ambako wote wako kwenye ziara rasmi. Wakati ambapo nchi zao mbili zinalaumiana kuhusiana na mzozo wa Syria na Ukraine, serikali zao zinarushiana cheche kwenye mitandao ya kijamii kuhusu nani wa kulaumiwa kwa mawaziri hao wawili kutofanya kikao Addis Ababa.
Urusi imesema kwamba Tillerson na Lavrov wote wanakaa katika hoteli ya kifahari ya Sheraton mjini Addis Ababa nchini Ethiopia ambapo Alhamis Tillerson atakuwa anakutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia anayeondoka madarakani pamoja na na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika.
Marekani haikupokea ombi la mkutano kutoka kwa serikali ya Urusi
Haijabainika mawaziri hao wawili walivyokosa kukutana huko Addis Ababa kwani Tillerson aliwasili Jumatano mchana wakati ambapo Lavrov aliondoka mjini humo Jumatano usiku na kuwasili Zimbabwe kituo cha pili cha ziara yake.
Pamoja na hayo Urusi inasema iliitisha mkutano na imeweka wazi kwamba ilituma ombi la kuwepo kwa mkutano hata kabla ya ziara hizo na imesisitiza kwamba ilituma ombi rasmi la kuweka miadi kwa Marekani ila inasema haikupokea jibu.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani Heather Nauert alisema wiki hii kwamba Marekani haijapokea ombi lolote la mkutano na Tillerson kutoka kwa serikali ya Urusi na kwamba haikuwa na tangazo lolote la mkutano.
Iwapo wangekutana kuna mengi ambayo wawakilishi hao wa nchi hizo mbili zenye nguvu duniani wangeyajadili. Nauert na Wizara ya Ulinzi ya Marekani wamekuwa wakiituhumu hadharani Urusi kwa vitendo vyake nchini Syria huku ikisema kwamba Urusi ndiyo inayowapiga raia kwa mabomu katika katika mji wa Ghouta mashariki ulioko karibu na Damascus.
Marekani na Urusi zashambuliana katika mitandao ya kijamii
"Mashambulizi huko Ghouta mashariki yanaonesha wazi kwamba Urusi haijali kabisa kuhusu mzozo wa kibinadamu ambao unaendelea kuongezeka," alisema Nauert, "raia bado wanashambuliwa kwa mabomu katika miji iliyoko nje ya Damascus," aliongeza msemaji huyo.
Ubalozi wa Urusi mjini Washington uliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba hii ingekuwa fursa nzuri ya kuzungumzia masuala muhimu ya kikanda na hata ya dunia nzima si kupitia vyombo vya habari bali kwa njia ya moja kwa moja. Urusi imeituhumu Marekani kwa kusambaza habari za uongo na kutoa taarifa zisizo za uhakika kuhusiana na uwezekano wa mkutano huo.
Nao ubalozi wa Urusi ukiilaumu Marekani katika mtandao wa kijamii wa Facebook umesema kusisitiza kwa Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani kwamba Urusi haikuitisha mkutano ni jambo linaloonesha kwamba kuna kitu fulani ambacho hakiendi sawa katika wizara hiyo.
Kwa upande wake Waziri Tillerson mbali na kuizuru Kenya, atazitembelea pia Djibouti, Nigeria na Chad.
Mwandishi: Jacob Safari/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman