1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu zote 16 zataja vikosi vyao vya AFCON

11 Januari 2013

Imesalia chini ya wiki moja tu, pazia la dimba maarufu zaidi barani Afrika likipandishwa nchini Afrika Kusini, kwa burudani la kabumbu ya kuwania kombe la mataifa ya Afrika AFCON

https://p.dw.com/p/17Hxd
Fans Suedafrika mit Fahnen und Vuvuzela - Troete Spiel 34: Frankreich - Suedafrika, Bloemfontein, 22.06.2010-- FIFA - Fussball Weltmeisterschaft 2010 in Suedafrika. Match 34: France - South Africa, Bloemfontein, 22th June 2010-- FIFA- Soccer World Championship 2010 in South Africa. JAPAN OUT!
Fans Suedafrika mit Fahnen und VuvuzelaPicha: picture alliance/augenklick/GES

Tayari vikosi vya timu zitakazoshiriki dimba hilo vimetajwa na Emmanuel Adebayor amejiumuishwa katika timu ya Togo, wakati mchezaji wa Mali, Mahamadou Diarra akitemwa nje. ADEBAYOR nahodha wa Togo alisema mwaka jana kwamba atasusia dimba hilo, akitaja sababu za usalama baada ya kuwa katika kikosi kilichoshambuliwa nchini Angola kabla ya dimba la mwaka wa 2010. mchezaji mmoja pamoja na afisa wa kikosi waliuawa na wanamgambo wanaopigania kujitenga eneo la Cabinda lenye utajiri wa mafuta, na Adebayor akanusurika kwa kujificha chini ya kiti cha basi lao. Klabu yake ya Tottehnam, Rais wa Togo, na maafisa wa soka ya kimataifa walilazimika kuingilia kati ili kumshawishi kujiunga na kikosi cha kocha Didier Six.

Nani atatamba na nani atazama?

Kwa kinyang’anyiro cha tano mfululizo, nahodha Didier Drogba na kikosi chake cha Cote d’Ivoire, chenye wachezaji wengi nyota ni lazima aubebe mzigo wa kupigiwa upatu wa kuwa timu bora ya kutwaa taji hilo, ambalo liliwaponyoka nchini Misri, Ghana, Angola na Gabon na Guinea ya Ikweta.

Didier Drogba na Christopher Katongo ni miongoni mwa majina maarufu katika soka ya Afrika
Didier Drogba na Christopher Katongo ni miongoni mwa majina maarufu katika soka ya AfrikaPicha: picture alliance/dpa

Wamewahi kulinusa kombe hilo mara mbili, kwa kushindwa kupitia mikwaju ya penalti kwa wenyeji Misri mjini Cairo miaka saba iliyopita, na mikononi mwa Zambia mjini Libreville mwaka jana. Aidha waliondolewa mara mbili katika nusu fainali na robo fainali.

Cote d’Ivoire wamewahi kutwaa taji hilo mara moja, kwa kuwabwaga Ghana mjini Dakar miaka 21 iliyopita katika fainali nyingine iliyoamuliwa kupitia mikwaju ya matuta, lakini hiyo ni zamani sana kabla ya kuchipuka kwa wachezaji Drogba, Kolo na Yaya Toure, Didier Zokora na Emmanuel Eboue. Cote d’Ivoire watakabana koo katika kundi D na mabingwa wa zamani Algeria na Tunisia na Togo.

Wakati Cote d'Ivoire ikionekana kuwa timu itakayotamba sana katika dimba hilo, kutokana na majina mazito ya wachezaji nyota wa ligi za Ulaya, kuna timu nyingine nyingi zenye uwezo wa kutia kibindoni zawadi ya dola milioni 1.5, ikiwa ni pamoja na Zambia, Algeria, Ghana, Mali, Morocco, Nigeria, Afrika Kusini na Tunisia. Angola na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo haipaswi kufutiliwa mbali pia. Timu kama vile Burkina Faso, Visiwa vya Cape Verde , Ethiopia, Niger na Togo ni timu nyingine tano ambazo zinaonekana kutokuwa na nafasi kubwa saana katika dimba hilo.

Klopp akiri kupoteza taji

Mkufunzi wa klabu ya Borussia Dortmund Jurgen Klopp tayari amekiri wkamba taji la Bundesliga limewaponyoka na kuwaendea Bayern munich. Klopp sasa amesema lengo lake ni Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bayern wana uongozi wa tofauti ya pointi 12 kileleni dhidi ya nambari tatu Dortmund, ambao wamekuwa mabingwa kwa misimu miwili iliyopita, na Klopp ambaye yuko mjini La Manga, Uhispania kwa mazoezi ya kabla ya mzunguko wa pili wa msimu amesema kwamba Bayern hawakamitiki kwa sasa. Klopp amefutilia mbali usajili wowote wa mchezaji mpya wakati huu wa mapumziko ya msimu wa baridi, akisema wataendelea na sera ya klabu hiyo kuwaimarisha chipukizi, badala ya kujaribu kushindana na Bayern katika kuwanunua wachezaji. Amesema uamuzi wa beki Sven Bender na beki Neven Subotic wa kuirefusha mikataba yao ni muhimu kwa klabu hiyo. Hata hivyo mchezaji ambaye hajaurefusha mkataba wake ni Robert Lewandowski. Mshambuliaji huyo wa Poland, anayemezewa mate na vilabu kadhaa vikuu, atakuwa huru kuhama mwishoni mwa msimu.

Jurgen Klopp anaangazia macho kabumbu ya jukwaa la Bara Ulaya
Jurgen Klopp anaangazia Jurmacho kabumbu ya jukwaa la Bara UlayaPicha: picture alliance/dpa

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters

Mhariri: Josephat Charo