1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Tokayaev apuuza mazungumzo na waandamanaji Kazakhstan

7 Januari 2022

Rais wa Kazakhstan amekataa miito ya mazungumzo na waandamanaji, baada ya siku kadhaa za machafuko, akiapa kuwasambaratisha "majambazi" wenye silaha, na kuviruhusu vikosi vya usalama kuua waandamanaji pasina kutoa onyo.

https://p.dw.com/p/45GiT
Proteste in Kasachstan | TV-Ansprache Präsident Toqajew
Picha: Kazakhstan's Presidential Press Service/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Kazakhstan amekataa miito ya mazungumzo na waandamanaji, baada ya siku kadhaa za machafuko yasio kifani, akiapa kuwasambaratisha wale aliowaita majambazi wenye silaha, huku akiviruhusu vikosi vya usalama kuua waandamanaji pasina kutoa onyo.

Katika hotuba kali kwa taifa, rais huyo Kassym-Jomart Tokayev pia ametoa shukran za kipekee kwa rais wa UrusiVladmir Putin, baada ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Moscow kutuma majeshi Kazakhstan kusaidia kutuliza machafuko.

Soma pia: Kiongozi wa Kazakhstan aviagiza vikosi kupiga riasi bila onyo

Vikosi vya usalama vilikuwa vimezuwia maeneo yote ya kimkakati ya Almaty, ambao ndiyo mji mkubwa zaidi na kitovu cha vurugu za karibuni, na mwandishi wa AFP amesema vilikuwa vinafyatua risasi hewani iwapo mtu yeyote alijaribu kusogea.

Kasachstan Bischkek Proteste vor Parlament
Watu wakiwa wamekusanyika mbele ya jengo la bunge la Kyrgyzstan kupinga uamuzi wa kupeleka wanajeshi nchini Kazakhstan, Januari 7, 2022.Picha: Abylai Saralayev/Tass/imago images

Kwingineko mji huo ulikuwa kama uliotelekezwa, huku mabenki, maduka ya vyakula na mikahawa vikiwa vimefungwa, na maduka machache yaliosalia wazi yakiwa yanaishiwa vyakula kwa kasi. Tokayev amesema hali ya utulivu imerejeshwa karibu kote nchini, huku akitupilia mbali miito ya kufanya majadiliano.

" Ni upuuzi gani huo! Ni aina gani ya majadiliano yanayoweza kufanywa na wahalifu, na wauaji? Tulilaazimika kushughulikia majambazi waliojihami barabara, wenye mafunzo, kutoka ndani na nje. Ni sahihi kabisaa, majambazi na magaidi. ndiyo maana wanapaswa kusambaratishwa, na hilo litafanyika hivi karibuni."

Ngome ya utulivu iliyovunjika

Ikitazamwa kwa muda mrefu kama taifa lenye utulivu zaidi miongoni mwa jamhuri za zamani za Kisovieti za Asia ya Kati, Kazakhstan, taifa lenye utajiri mkubwa wa nishati, inakabiliwa na mzozo wake mkubwa zaidi katika miongo kadhaa. Waandamanaji walivamia majengo ya serikali mjini Almaty siku ya Jumatano, na kupambana na polisi na jeshi.

Soma pia:Vurugu zazuka upya Kazakhstan baada ya Urusi kutuma askari 

Wizara ya mambo ya ndani imesema wahalifu 26 wenye silaha wameuawa katika machafuko hayo, baada ya hapo awali kuripoti dazeni kadhaa za vifo. Imesema maafisa 18 wa usalama wameuawa pia, na zaidi ya 740 kujeruhiwa, na zaidi ya watu 3,800 wamekamatwa.

Almaty, Kasachstan | Schwere Unruhen
Vikosi vya usalama vikitumiwa kuzima maandamano ya umma dhidi ya serikali mjini Almaty, Kazakhstan, Januari 6, 2022.Picha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Rais wa Urusi Vladmir Putin amezungumza na washirika wa kanda ya Asia ya Kati kujadili machafuko hayo. Ikulu ya Kremlin imesema Putin amezungumza mara kadhaa kwa njia ya simu na rais Tokayev, pamoja na viongozi wengine wa mataifa yanayounda shirika la la ushirikiano wa kiusalama, ambao ni muungano wa jamhuri kadhaa za zamani za kisovieti unaodhibitiwa Urusi.

Haijabainika wazi ni wanajeshi wangapi wametumwa katika kikosi cha muungano huo, ambacho kinajumlisha vikosi kutoka Urusi, Belarus, Armenia, Tajikstan na Kyrgyzstan, lakini vyombo vya habari mjini Moscow, vimesema kikosi cha Urusi kinatarajiwa kuwa chini ya wanajeshi 5,000.

Chanzo: Mashirika