TPSF yafurahishwa na mwanzo mpya wa Rais Samia Hassan
7 Aprili 2021Taasisi ya sekta binafsi nchini Tanzania TPSF imeelezea kufurahishwa na mwanzo mpya wa rais samia suluhu Hassan kutokana na kuweka wazi dhamira yake juu ya wawekezaji, kadhalika kuitaka mamlaka kutunga sera ya maendeleo kuhusu sekta hiyo.
Siku moja baada ya rais Samia Suluhu kuweka bayana dhima yake ya kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi kwa namna inayozinufaisha pande zote, wadau wa sekta hiyo wametoka hadharani na kupongeza uamuzi huo wa mamalaka, huku wakiahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika kufikia malengo ya kiuchumi.
Katibu mtendaji wa TPSF Fransis Nanai amesema falsafa inayotumiwa na awamu hii inalenga kuvutia wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni na hata kuwarudisha wale waliofunga biashara zao kutokana na vikwazo kadhaa, ikiwemo vile vilivyosababishwa na baadhi ya watendaji serikali.
TPSF yatoa wito wa ushirikiano ili kuvutia wawekezaji zaidi
Amesema ni vyema serikali kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kutunga sera ambayo mbali na mambo mengine itaipatia taasisi hiyo mamlaka ya kisheria katika kuwahudumia wananchama wake, ambapo hivi sasa wawekezaji wengi wanaingia kwa hiyari na si kwa matakwa ya kisheria. Alisisitiza "Tutafanya kazi kwa uwazi, kwa ukweli, ueledi na uaminifu. Hizi ndizo tunu au vigezo ambavyo vitatufanya tuaminiwe na serikali. Lakini pia tuna ombi kwa serikali kwamba watukee mayingira mazuri ya kufanya biashara, na kupata sera ya maendeleo ya sekta binafsi, tuna imani kwamba kukiwa na sera yetu binfasi, inayotuhusu sisi, itaweza ndani ya sera hiyo kuipatia TPSF uwezo kuwaongoza na kuwasimia wanachama wake."
Wakati taifa hilo la Afrika Mashariki likitangazwa kuingia uchumi wa kati wa kiwango cha chini mwaka uliopita, sekta binafsi inatajwa kutoa mchango mkubwa katika kukuza pato la watu binafsi ikienda sambamba na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kiuchumi kwa upande wao waona mbali na pande mbili hizi kuonesha dhima ya kuanza upya kwa maridhiano sasa ni wakati wa serikali kuanzisha mkakati mpana wa kiuchumi, mkakati wa kibiashara unaowalinda wawekezaji ili kuwa na uwekezaji endelevu na wenye tija kwa umma. Bravious Kahoza mchambuzi wa masuala ya kiuchumi.
"Jambo ambalo serikali inahitaji kulitilia umuhimu ni kutengeneza kitengo cha kiintelijensia ambacho kinaweza kuwa kinapata taarifa za kitu gani kinatokea katika sekta za kiuwekezaji na katika mazingira mapana ya ndani na nje ya nchi ili kuepuka kuweka mazingira ya kiuwekezaji ambayo yanakinzana sana na taratibu za kiuwekezaji katika maeneo yetu au duniani kwa ujumla".
Hii ni mara ya pili kwa sekts binafsi kutoa ombi kwa serikali kuweka mazingira wezeshi kwa biashara nchini, mara ya kwanza ikiwa mwanzoni mwa mwaka huu wakati wa utawala wa hayati Dk. John Magufuli. Jana rais Samia Suluhu Hassana alikiri kwa mara ya kwanza kwamba hali ya kiuchumi nchini humo ni mbaya, na kuwataka watendaji wa serikali kurahisisha mazingira kwa wawekezaji wa ndani na nje.