Traore atangaza mipango yake Mali
30 Julai 2012Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na televisheni ya taifa, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 70, alitangaza mipango kuhusu serikali ya mpito atakayoongoza, mpangilio ambao unakuja baada ya maafisa wa ngazi ya chini kumpindua rais aliyechaguliwa kidemokrasia mwezi Machi, wiki chache kabla ya uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa.
Mnamo mwezi Mei, rais huyo wa mpito alipigwa hadi akapoteza fahamu na kundi la waandamanaji wanaomuunga mkono kiongozi wa mapinduzi, ambaye siku chache kabla alikuwa amesaini muafaka wa kuwachia madaraka.
Traore alisema nchi hiyo itaongozwa na Baraza Kuu, linalomjumuisha yeye na Makamu wake wawili. Mmoja wa makamu wa rais atasimamia kamati ambayo italeta mageuzi jeshini na pia kushughulikia upande wa Kaskazini mwa nchi hiyo ambao ulitwaliwa na waasi wa Kiislamu wenye itikadi kali baada ya kufanyika mapinduzi. Alisema kamati pia itaundwa kujaribu kuzungumza na makundi yenye silaha katika upande wa kaskazini ili kutafuta amani.
Makundi ya kiislamu hajayataja
Ijapokuwa Traore hakutaja Ansar Dine, ambalo ni kundi kuu la Kiislamu linalodhibiti upande wa Kaskazini, taarifa yake ilionekana kuashiria kuwa serikali ya Mali iko tayari kufanya mazungumzo na kundi hilo lenye mafungamano na al-Qaeda.
Katika hotuba hiyo, aliwataka Wamali wasameheane na kuungana katika juhudi za kumaliza mgogoro wa kisiasa katika upande wa Kaskazini, na kuiunganisha nchi hiyo.
Traore alisema katika hotuba yake kuwa atafanya mazungumzo ya kuundwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa, lakini hakueleza kuhusu ratiba ya kutimiza hilo.
Diarra asema hataondoka madarakani
Waziri Mkuu, Cheick Modibo Diarra, katika hotuba yake iliyorushwa kupitia televisheni siku moja kabla, alisema atasalia madarakani ili kumaliza kazi yake. Alisema hatajiuzulu na hawezi kujiuzulu kwa sababu wanahitaji muda wa kujiandaa kama viongozi na kuwaondoa wanamgambo wanaodhibiti upande wa Kaskazini.
Kambi inayounga mkono mapinduzi inamtaka Diarra kubakia, na inapinga pendekezo la jeshi la kigeni kuingilia kati katika mzozo wa nchi hiyo. Wafuasi wa Waziri huyo Mkuu walifanya mkutano jumapili wakimtaka asimame kidete.
Rais wa Cote d'Ivoire, Alassane Ouattara, ambaye ni rais wa sasa wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, aliliambia gazeti moja la kila wiki nchini Ufaransa, Journal du Dimanche, kuwa jumuiya hiyo inajiandaa kuwasilisha ombi jipya kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kujiingiza kijeshi nchini Mali.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/dpa
Mhariri: Othman, Miraji